***********************
Jeshi la Polisi mikoa ya nyanda za juu kusini yaani Njombe, Mbeya na Iringa, kwa kipindi cha kuanzia Machi 12, 2023 hadi Machi 23, 2023 limefanikiwa kukamata watuhumiwa 87 wa matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwemo, unyanganyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvunja ofisi usiku na kuiba, kupatikana na mali za wizi, kupatikana na pombe moshi na kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi na mirungi.
Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na mikoa ya Mbeya na Iringa limefanikiwa kuwamata watuhumiwa waliohusika na tukio la unyanganyi wa kutumia silaha huko Luponde mkoani Njombe kwa kutega magogo barabarani na kisha kupora fedha za wafanyabiashara.
Akielezea mafanikio hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe ACP HAMIS ISSAH ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu kusini amesema ushirikiano mzuri wa mikoa ya Iringa na Mbeya imefanikisha kuwakamata watuhumiwa hao 87 ambao wamekuwa wakifanya matukio mbalimbali na kukimbilia mikoa mingine ya jirani.
Aidha amesema kupitia operesheni na misako ya mikoa mitatu vitu mbalimbali ambavyo viliibwa na kuporwa katika matukio mbalimbali vimekamatwa amabvyo ni:-
- Gari moja aina ya Nissan X TRAIL namba T. T.571 DXS rangi nyeusi
- Pikipiki 08 za aina mbalimbali ikiwemo iliyoibiwa Chamwino Dodoma
- Dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa kilogramu 118.
- Pombe ya Moshi @ Gongo ujazo wa lita 60
- TV Flat Screen 05 za aina na ukubwa mbalimbali.
- Laptop 04
- Desktop 04
- Simu za mkononi 22 za aina mbalimbali
- Betri za gari 18
- Betri za Solar 02
- Sub-woofer 04
- Vifaa mbalimbali za Hospitalini.
- Nyara za serikali (Meno ya Tembo) 02.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya ACP BANJAMINI KUZAGA amesema kuwa uhalifu unaojitokeza sasa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya nyanda za juu kusini ni kutokana na kuwepo kwa miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ya ujenzi wa barabara ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakifika kwa ajili ya kutafuta ajira lakini baadhi yao ujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu kama vile utekaji na unyang’anyi wa kutumia silaha. Hata hivyo, amewatahadharisha kuwa Jeshi la Polisi halitasita kupambana nao na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa ACP ALLAN BUKUMBI amesema kuwa ushirikiano ndio unajenga msingi wa kazi kwa umoja wetu akasisitiza kuwa watuhumiwa wengi wamekamatwa mikoa ya jirani kutokana na kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kikosi kazi kilichoundwa kufanya kazi kwa kushirikiana.
Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Kamanda ISSAH amesema, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu ya Polisi jamii ili wananchi wajue na kuwa na uelewa wa namna ya kudhibiti, kuzuia na kutanzua uhalifu katika maeneo yao ikiwemo kutoa taarifa za uhalifu, wahalifu na zile za ukatili wa kijinsia
Pia ametoa wito kwa jamii kwa wale wote wanaojihusisha na uhalifu waache mara moja kwani Jeshi la Polisi lipo makini na halitosita kuchukua hatua kwa mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uhalifu.
Mafanikio haya yamekuja kufuatilia kikao kazi cha makamanda wa mikoa ya nyanda za juu kusini kilichokaa Machi 11, 2023 Jijini Mbeya ambacho kiliweka mpango kazi madhubuti wa kuzuia na kutanzua uhalifu ikiwa ni Pamoja na kufanya operesheni na misako ya pamoja na kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu.