************
Jumla ya Shilingi 223,917,101,547.11 zimepelekwa wilaya ya Tunduru kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo tangu mwezi Machi 2021 – Machi 2023, miaka 2 ambayo serikali ya Tanzania imeongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro ameeleza hayo wakati wa Kongamano la Kiwilaya la kuadhimisha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita lililofanyika katika ukumbi wa Cluster wilayani Tunduru leo.
DC Mtatiro ameeleza kuwa mradi wa kipekee na kihistoria ambao umetia fora ni ule wa Shilingi Bilioni 150 ambazo zimepelekwa wilayani humo kukamilisha ujenzi wa Msongo Mkubwa wa umeme wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru wenye urefu wa kilomita 210, mradi ambao utamaliza kabisa matatizo ya umeme wilayani Tunduru na ambao utakamilika ndani ya miezi 15 huku Wakandarasi wakiwa wamesharipoti wilayani humo.
Miradi mingine iliyopeleka fedha nyingi wilayani Tunduru ni REA Shilingi Bilioni 31.9, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Shilingi Bilioni 9.6, Barabara Vijijini Shilingi Bilioni 8, Miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari Shilingi Bilioni 7.4, Miundombinu ya Sekta ya Afya Shilingi Bilioni 3.1, Miundombinu ya Maji Shilingi Bilioni 5.2, Kilimo na Ushirika Bilioni 4.5, Elimu Bila Malipo Shilingi Bilioni 1.5.
DC Mtatiro amewaasa wananchi wa Tunduru kuitunza miundombinu yote inayojengwa wilayani humo na kuitumia kwa faida ya kuendeleza uchumi wa familia na taifa ili kila kizazi kipate manufaa.
DC Mtatiro amesisitiza watumishi wote wa serikali kuendelea kutumia kila shilingi inayofikishwa Tunduru kwa uaminifu mkubwa ili kuleta tija ya muda mrefu na amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika wilaya hiyo ya pembezoni mwa nchi fedha nyingi zaidi kuliko awamu zote za serikali za Tanzania.
Akitoa pongezi katika kongamano hilo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Said Bwanali amesema Rais Samia anatimiza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ipasavyo na ameitendea haki wilaya hiyo.
Idd M. Mohamed,
Tunduru.