Na John Walter-Manyara
Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Manyara imeanza kwa kasi kwa kutoa elimu ya Kujitambua kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, kujua Ukatili na kuripoti wanapofanyiwa au kuona mtu akifanyiwa Ukatili.
Katibu wa SMAUJATA mkoa wa Manyara ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la jinsia Mkoa, Willnes Kimario amewataka wanafunzi kuwafichua wazazi ,walezi na wote wanaofanya ukatili dhidi yao.
Pia amewataka wakawe mabalozi kwa wazazi wao kuwaambia juu ya madhara ya Ukeketaji na Ukatili mwingine kama walivyofundishwa.
Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Babati Agatha Patrice amewaasa wanafunzi wasiwe rahisi kukubali lifti wanazopewa barabarani au Chipsi kwani ndo chanzo Cha kufanyiwa Ukatili na kukatisha masomo yao.
Amesema Mtoto wa kike na wa Kiume wote wana haki sawa na wanapaswa kulindwa.
Amesema jamii ikishirikiana vyema na wadau wa kupinga Ukatili pamoja na jeshi la polisi itaongeza nguvu katika kupunguza vitendo hivyo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Babati Philipo Sulle, amesema upo Ukatili ambao unafanywa pia na Wanafunzi wenyewe kwa wenyewe ukiwemo Ukatili wa kihisia kwa kusemana vibaya na kuwaonya wenye tabia hiyo waache mara Moja.
Ametoa wito kwa wazazi kuongeza usimamizi wa karibu kwa watoto wao ili kuwaepusha na matukio hayo na walimu kuendelea kusisitiza maadili mema yanayofuata tamaduni za Kitanzania.
Mkuu wa shule ya Sekondari Dabil Alfred Sulle, amesema licha ya shule hiyo kutokuwa Mhanga wa Ukatili lakini shule nyingi Za Kata ya Dabil zinatajwa kuwa na Wanafunzi waliokumbana na adha ya Ukatili wa aina mbalimbali.
Mkuu Dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya Babati mkaguzi msaidizi wa polisi Daudi Danyesi amewataka wanafunzi na wananchi kwa Ujumla kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili wahusika wakamatwe na washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Wanafunzi wameshukuru kwa elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri Kwa jamii.
Mkoa wa Manyara kitakwimu katika Ukatili wa kikinsia unatajwa kushika nafasi ya pili huku kwa Ukeketaji ukishika nafasi ya kwanza Kitaifa.
Ukanda wa Tarafa ya Bashnet ndo unaotajwa kuongoza kwa vitendo vya Ukatili huku kesi zikimalizwa kinyumbani.
SMAUJATA Manyara wametoa elimu hiyo katika Shule tano za wilaya ya Babati Dabil Sekondari, shule ya Msingi Mandi, Shule ya Msingi Barmot, Shule ya Msingi Sabilo na Shule ya Msingi Lomhong.