Baadhi ya wanafunzi wa darasa la Awali wakiendelea kujifunza ikiwa ni hatua yao ya awali katika elimu ya msingi.
KUANZISHWA kwa shule shikizi tisa katika Manispaa ya Singida kumetajwa kuwa
ni mwarobaini kwa watoto walio chini ya miaka minane kutembea umbali wa zaidi
ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu kwenye shule mama, kuimarisha ulinzi na
usalama wao na kupunguza utoro na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje alibainisha hayo
wakati akizungumzia mafanikio na changamoto za shule shikizi katika halmashauri
hiyo.
“Kuanzia mwaka 2017 hadi sasa, tumefanikiwa kuwa na shule shikizi tisa
ambazo kwa kweli zimesaidia watoto wadogo; hasa wa chekechea, wa darasa la
kwanza na la pili kutembea umbali mrefu
kutafuta elimu; hivyo kumaliza utoro, vitendo vya ukatili wa kijinsia njiani au
usalama wao kuwa mashakani wanapokutana na wanyama kama fisi” alisema.
Alieleza kuwa baadhi ya shule za msingi mama zipo umbali wa kilomita 5;
hivyo ilikuwa vigumu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka minane kutembea
umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu; hivyo Manispaa kuamua
kuanzisha shule shikizi jirani na makazi ya watu kuondoa changamoto hiyo.
Maje alizitaja shule hizo Shikizi kuwa ni pamoja na Mnung’una, Mughenyi,
Manguampyughu, Sundu, Mwembemoja, Mwachichi, Nkuhi, Mwaghumpi na Makyunje ambazo
hadi hivi sasa zina jumla ya wanafunzi 2,665 kati yao wavulana ni 1,316 na
wasichana 1,349.
Alisema kuwa kuendelezwa kwa shule hizo ni sehemu ya utekelezaji wa
Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
ya mwaka 2021, ambayo pamoja na mambo mengine, inaweka mkazo zaidi kwenye
kuimarisha ulinzi na usalama, afya, lishe bora, elimu na malezi yenye mwitikio
kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8.
Hata hivyo; anakiri kuwa bado shule hizo shikizi zinakabiliwa na changamoto
mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na
miundombinu ya kutosha kama madarasa, vyoo na nyumba za walimu huku zikiwa
hazina fungu la uendeshaji hivyo kuendelea kutegemea fungu lililoko shule mama
na hakuna walimu wa kudumu kwani walimu wake hutegemea zaidi kutoka shule mama
na wale wa kujitolea.
Baadhi ya wazazi na walezi wanaipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa
kuanzisha shule shikizi ili kupunguza
changamoto kwa watoto na kuomba ziboreshwe na kusajiliwa kuwa shule kamili.
“Mimi mtoto wangu aliponea pale Mwembemoja ndio ikawa nafuu; vinginevyo
ilikuwa aache shule kabisa au nimtafutie hizi za kuchukuliwa na magari maana
mtoto alikuwa akitembea zaidi ya kilomita saba kwenda tu bado kurudi, akija
nyumbani amechoka mpaka basi” alisema Halima Ali mkazi wa Mtipa Singida na
kuongeza kuwa sasa shule hiyo imepata usajili kamili.
Naye, Ibrahimu Loth mkazi wa Mwenge anapongeza kuanzishwa kwa shule hizo
shikizi kwani kwa dunia ya sasa watoto wadogo kutembea umbali mrefu ni hatari
kwani wanaweza kufanyiwa vitendo
vya ukatili ikiwemo ulawiti, kubakwa au kujeruhiwa na wanyama.
Walimu wa shule za awali na msingi katika Manispaa ya Singida
wanasema kuwa shule shikizi zinaweza
kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwani awali watoto walikuwa wanafika shule
wakiwa wamechoka kwa kutembea umbali mrefu na muda wote wakipiga miayo tu
darasani kwa uchovu na njaa.
“Mengine huwa hatusemi tu ingawa tunaumia maana na sisi pia ni wazazi.
Ukipewa kufundisha darasa la awali na la kwanza duh! ikifika saa 4 asubuhi
watoto wote wanaotoka mbali unakuta
wanachapa usingizi darasani na walio macho ni miayo kwa kwenda mbele, ila sasa
kwa hizi shikizi watoto hawatembei umbali mrefu hivyo hawachoki, tunaishukuru
Serikali” alisema mmoja wa walimu hao.
Kulingana na taarifa za idara ya
elimu Manispaa ya Singida, kati ya shule 9 shikizi zilizoanzishwa, shule 5 tayari zimesajiliwa na Wizara ya
elimu kuwa shule kamili huku nyingine zikiwa kwenye mchakato wa kusajiliwa.
Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje akiwa kwenye moja ya vikao vyake kuelezea umuhimu wa Shule Shikizi |