Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAKALA wa usambazaji maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani, unakisia kupokea na kutumia kiasi cha sh.bilioni 1.705.129.276 katika bajeti ya mwaka 2023/2024.
Kati ya fedha hizo milioni 25.395 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya ofisi na bilioni 1.679.734.276 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wa PforR na NWF.
Akielezea kuhusu mpango wa bajeti ya mwaka 2023/2024 , kwa madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Mji huo, Meneja wa RUWASA Bagamoyo, James Kionaumela alieleza kuwa, maandalizi ya mpango wa bajeti hiyo umezingatia muongozo wa mpango wa bajeti,ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, maagizo mbalimbali ya viongozi na ukomo wa bajeti uliotolewa.
Aidha alieleza, jukumu kubwa walilojipanga nalo ni kuendelea kuwezesha wananchi Vijijini kupata maji safi,salama na ya kuhakika katika umbali usiozidi mita 400 kwa mahitaji Yao binafsi na mahitaji ya kiuchumi.
“Mpango huu wa bajeti 2023/2024 unahusu ujenzi wa miradi mipya ya maji, usimamizi na uendelevu wa miradi, ukarabati na matengenezo ya miradi ya maji iliyoharibika na bajeti ya matumizi mengine inayohusu shughuli za kila siku za ofisi “: alifafanua Kionaumela.
Vilevile Kionaumela alielezea kwamba, utekelezaji wa mpango huo unategemea fedha kutoka kwa wahisani wa Maendeleo kupitia mfuko wa maji NWF pamoja ulio chini ya programu ya payment for result (PforR )na mapato ya ndani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Mohammed Usinga aliitaka, RUWASA na DAWASA kusimamia wakandarasi wa miradi inayoendelea kutekelezwa kwenye maeneo mbalimbali ili waweze kukamilisha kwa wakati kulingana na mikataba yao ili kutimiza malengo ya Serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika kwa jamii.
“Serikali inafanya jitihada kubwa kutenga fedha nyingi ili kuondoa kero ya maji mijini na Vijijini, hivyo ni wakati wenu RUWASA na DAWASA kusimamia kikamilifu wakandarasi waweze kwenda na kasi ya matakwa ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anaondoa kero hiyo ya maji”alisema Usinga.