Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Handeni mkoani Tanga alipokwenda kukabidhi hatimilki za ardhi wakati wa ziara ya siku moja katika halmashauri ya Mji wa Handeni na kijiji cha Msomera tarehe 22 Machi 2023. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando akizungumza wakati Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kukabidhi hati milki za ardhi wilayani Handeni mkoani Tanga tarehe 22 Machi 2023. Kulia ni Katibu Tawala wilaya ya Handeni Mashaka Mugeta
Sehemu ya wananchi wa Handeni waliojitokeza kukabidhiwa hati milki za ardhi na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 22 Machi 2023.
Waziri wa Ardhi Nyimba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati milki ya Ardhi pamoja na mche wa mti mkazi wa Handeni Doto Bakari alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo tarehe 22 Machi 2023.
Afisa kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) akitoa elimu ya upandaji miti kwa wananchi wa handeni waliokabidhiwa hati milki za ardhi na Waziri wa Ardhi Nyimba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 22 Machi 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
*****************************
Na Munir Shemweta, WANMM HANDENI
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi waliokabidhiwa hati milki za ardhi wilayani Handeni mkoani Tanga kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo yao ikiwa ni moja ya sharti lililopo katika hati ya ardhi.
Dkt Mabula ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Machi 2023 wilayani Handeni Mkoani Tanga wakati akikabidhi hati milki za ardhi kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni.
Amesema, katika kuhakikisha maeneo wanayomilikishwa yanakuwa na utunzaji mzuri wa mazingira wizara yake imeona ije na sharti la kuwataka wanaomilikishwa kupanda miti mitano katika eneo wanalomilikishwa ili kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi hukata miti kwa visingizio vya matumizi mbalimbali jambo linalosababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali.
Amebainisha kuwa, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa dhidi ya uharibifu huo wa mazingirs kuna hatari ya vizazi vijavyo kukumbwa na ukame ama majira ya mvua kubadilika badilika.
“Tunahitaji kutunza mazingira katika maeneo yetu kwa kupanda miti ya matunda ili tupendezeshe mandhari ya maeneo yetu” alisema Dkt Mabula.
Aidha, Waziri Mabula amewataka wazazi kuwafundisha watoto wao namna bora ya kupanda miti na kuitunza kwa lengo la kuwajenga kiakili kuhusiana na utunzaji wa mazingira.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka wananchi waliokabidhiwa hati kuhakikisha wanafuata masharti ya umiliki ardhi ikiwemo kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni.
Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando alimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kuwa, wilaya yake imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuhakikisha inatatua kero za wananchi ziliwemo zile za ardhi na moja ya mikakati iliyopo ni kuwa na kliniki inayozunguka kwa lengo la kutatua kero za wananchi.