KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, akikagua maendeleo ya wanafunzi wa kozi ya komputa katika Chuo cha Mwenge Community College kinachomilikiwa na CCM kilichopo Amani Mkoa Unguja, katika ziara yake chuoni hapo.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis(kulia),akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Televisheni mtandao cha Al-fatah TV Rashid Saleh huko hapo Amani msikitini katika ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akikabidhiwa taarifa mbalimbali za kiutendaji za Chuo cha MCC na Mwenge FM, katika ziara yake ya kutembelea Chuo hicho.
***********************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amesema ameridhishwa na ushirikiano wa vyombo vya habari nchini katika kutangaza na kuripoti matukio na habari za utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifanya tathmini ya ziara yake katika vyombo vya habari nchini hapo Kisiwandui Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Alisema licha ya vyombo vya habari kukabiliwa na changamoto mbalimbali vimekuwa vikitekeleza wajibu wake wa kuhabarisha,kuburudisha,kuhamasisha na kuhubiri umoja na mshikamano.
“Lengo la ziara hii ni kudumisha ushirikiano na vyombo vya habari nchini ambavyo ni wadau wetu muhimu katika shughuli zetu za kisiasa na kisera.
Nachukua fursa hii kuwasihi viongozi wa Serikali na Chama wenye dhamana ya kusema na kutoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM watoe ushirikiano kwa vyombo vya habari ili wananchi wa mijini na vijijini wajue miradi na fursa zinazotekelezwa na serikali zao.”, alisema Mbeto.
Aliwapongeza waandishi wa habari na kuongeza kuwa wanafanya kazi kubwa kupitia kalamu zao za kuhamasisha na kuhabarisha jamii juu ya masuala ya kiuchumi,kijamii,kisisa na kimaendeleo.
Pamoja na hayo alisema tofauti ya Chama Cha Mapinduzi na vyama vingine vya kisiasa ni kuwa na mfumo wake imara wa demokrasia,unaotoa fursa kwa kila mwanachama mwenye sifa kuwa kiongozi kutokana na nafasi anayowania.
Alisema, mfumo huo ndio unaojenga mabadiliko ya kiungozi kila baada ya miaka kumi kupatikana viongozi wapya ndani ya serikali, na kila baada ya miaka mitano kupatikana viongozi wapya ndani ya CCM.
Katibu huyo Mbeto, alielea kuwa nguvu ya kisiasa ya chama hicho inaanzia katika mfumo wa ngazi za mashina na kupanda hadi taifa wanapofanya maamuzi kwa kufuata utaratibu wa vikao.
Mbeto, aliweka wazi kuwa hakuna chama cha kisiasa nchini kinachofuata utaratibu huo kama wa CCM na badala yake wanateuana na kupeana nafasi za uongozi kwa kufuata misingi ya ukabila,ukanda na umaarufu hali ambayo hawawezi kupata viongozi imara na wenye maono ya kuongoza Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Katika maelezo yake Katibu huyo alikiri kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuamini kuwa siasa za maridhiano ndizo zinazoijenga Zanzibar kimaendeleo.
“Katika hili mie mwenyewe nilikwenda kwenye mkutano wa ACT-Wazalendo nilialikwa tukaona ndio fursa ya sisi kwenda kuwafundisha wenzetu kuwa sasa CCM haioni kama upinzani ni kama uadui,”alisema
Alisema CCM inaiona upinzani kama sehemu ya kujitathmini katika mapungufu yake na kuielezea serikali zinazoiunda.
“Sisi CCM tunataka kuonyesha kuwa sisi hatuna tatizo katika siasa kutakuwa na tatizo endapo pale wapinzani wanayatumia vibaya majukwa ya kisiasa kwa kuwatukana viongozi ama kupotosha ukweli wa mambo,”alisema
Katika maelezo yake alisema baada ya yeye Katibu kuhudhuria katika mkutano huo ndipo akamuona Rais Samia Suluhu Hassan pia akihudhuria mkutano wa wanawake wa chama cha CHADEMA.
Alisema serikali za CCM zimefanya mambo mengi na kwamba hakuna jambo ambalo wanachama cha CCM hawatoweza kujibu kwa hoja kutokana na mambo hayo yaliofanywa na chama.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Al-fatah TV Rashid Salim,alisema kuwa utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 umeleta ufanisi katika sekta ya habari, ambapo kwa sasa wamekuwa wakitangaza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika risala iliyowasilishwa na Kituo cha redio ya Mwenge FM kinachomilikiwa na CCM wamesema wanakabiliwa na changamoto za udogo wa kifaa cha kurusha matangazo ambacho kwa sasa hakikidhi mahitaji yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha uandishi wa habari cha Mwenge Community, Saleh Koshuma, alisema chuo hicho kina changamoto ya kusitishiwa usajili wa chuo kutoka NACTE.
“Uongozi wa chuo kimeanza kuchukua hatua mbalimbali ya kukamilisha usajili wa chuo lakini pia changamoto nyingine ni vifaa vya kufundishia,”alisema.
Ziara hiyo imehitimishwa katika Vituo vya Bomba FM,Sunet TV,Al-fatah TV na Mwenge FM ambapo Katibu huyo ataendelea na ziara yake baada ya kumaliza mwezi wa Ramadhani.