Na Mwandishi wetu, Babati
MKOA wa Manyara na Halmashauri zake umeomba kupitishiwa sh184.7 bilioni kwa ajili ya makadirio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 za miradi mbalimbali ya maendeleo na matumizi mengine.
Kati ya fedha hizo sh70 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mipango 40 ya miradi ya maendeleo kwenye mkoa huo na halmashauri zake saba za Babati mjini, Babati wilaya, Mbulu mjini, Mbulu wilaya, Simanjiro, Hanang’ na Kiteto.
Katibu Tawala msaidizi wa mkoa wa Manyara, (mipango na uratibu) Maarufu Mkwaya ameyasema hayo wakati akisoma mpango huo wa bajeti mjini Babati katika kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC).
Maarufu amesema shughuli za maendeleo zitakazotekelezwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa ni ujenzi wa ofisi za wakuu wa wilaya za Babati na Kitengo na kufanya ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba za makazi ya makatibu tawala wa wilaya za Mbulu na Simanjiro.
Amesema pia wamelenga kutembea, kushauri na kusaidia miradi ya kiuchumi na kijamii ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa na kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa uhaurishaji wa fedha kwa kaya maskini katika maeneo yatakayonufaika na mpango wa Tasaf.
“Tunatarajia pia kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi inayotekelezwa na mamlaka za serikali za mitaa ndani ya mkoa wa Manyara kupitia halmashauri zake saba za wilaya,” amesema Maarufu.
Amesema wanatarajia kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa utoaji wa huduma za elimu, usafi wa mazingira na utoaji wa huduma za afya kwa mkoa wa Manyara.
Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoa wa Manyara, mhanidisi Walter Kirita amesema katika mpango wa bajeti yao kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 wameomba kuidhinishiwa kiasi cha sh20.5 bilioni.
Kaimu meneja wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Manyara, mhandisi Dutu Masele amesema kwa upande wao wameomba kupitishiwa kiasi cha sh11 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.