Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKURUGENZI wa shirika lisilo la kiserikali la Civil Society Protection Foundation (CSP) Nemency Iriya amesema wanaendelea kufuatilia mradi wa Tanzanite na uchumi imara wa mwanamke unaotarajia kunufaisha kata tatu za Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.
Iriya amesema wanaendelea kufuatilia mradi huo ambao lengo ni kuwanufaisha wanawake wajasiriamali wa madini ya Tanzanite waliopo kwenye kata tatu za Mirerani, Endiamtu na Naisinyai.
Amesema wamezindua mradi huo ambao umelenga kuhakikisha kuwa wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite wanafanya kazi zao kwa ufanisi.
“Tunatarajia wanawake hao watafanya biashara zao kwa amani, uhuru na faida, kwani mara baada ya kujengwa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Amesema eneo hilo hakuna magari ya abiria hivyo kuna changamoto ya usafiri kwani usafiri uliopo ni wa kupanda pikipiki maarufu kama bodaboda ambayo unalipia shilingi 3,000 na pia upekuzi usio na stara unaodhalilisha.
Amesema upekuzi huo unasababisha wanawake hao wajasiriamali hasa wenye umri mkubwa kuvuliwa nguo na kupekuliwa na askari wenye umri mdogo, unasababisha udhalilishaji huo.
“Walengwa wa mradi huu ni wanawake wanaofanya biashara ndogo ndogo kwenye machimbo ya Tanzanite, viongozi wa vitongoji, wa kata na afisa madini mkazi (RMO) wa Mirerani,” amesema Iriya.