Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul – Wakil, Zanzibar,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita akizungumza wakati alipomkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufunga Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Zanzibar
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea tuzo ya kukienzi Kiswahili baada ya kufunga Kongomano la Idhaa za Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul – Wakil, Zanzibar
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani baada ya kufunga Kongamano hilo kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Zanzibar Machi 19, 2023. Kulia kwake ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita na kushoto ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari na wadau wote wa Kiswahili waweke mkakati wa pamoja wa kuitangaza lugha hiyo nje ya nchi.
Mbali na kuitangaza lugha hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amehimiza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, kuweka mkakati wa kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa na kuhakikisha kuwa maelezo ya matumizi ya bidhaa yanawekwa kwa Kiswahili.
Ametoa wito huo jana usiku (Jumapili, Machi 19, 2023) wakati akizungumza na wadau mbalimbali alipokuwa akifunga Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Kikwajuni, Zanzibar.
Akisisitiza jukumu la kuhakikisha matumizi ya lugha ya Kiswahili yanavuka mipaka ya nchi, Waziri Mkuu alisema: “Nitoe rai kwa waandishi wa habari kuimarisha ushirikiano na wataalamu wa Kiswahili na taasisi za Kiswahili kuhakikisha kwamba mnaweka mikakati thabiti ya kupenyeza Kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali.”
Akielezea umuhimu wa kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, Waziri Mkuu alisema tafiti zina tabia ya kueleza changamoto na kutafuta majibu. “Kwa hiyo tufanye tafiti, BAKIZA na BAKITA tutumie vyuo vikuu kufanya tafiti na kubainisha majibu haya. Tutumie vizuri fursa ya UNESCO ya tarehe 7 Julai, kila mwaka kwa kuendesha makongamano na kubainisha suluhisho,” alisisitiza.
Akielezea mikakati ya kukibidhaisha Kiswahili, Waziri Mkuu alisema iko fursa ya nchi jirani za Malawi, Msumbiji, Sudan na Congo ambako walimu wanaweza kupata ajira za kufundisha lugha hiyo. “Lazima tujitafakari ni kwa nini Kiswahili kinaenda nchi za jirani lakini walimu wengi wa Kiswahili hawatoki Tanzania Bara au Zanzibar wakati Kiswahili kimezaliwa hapa hapa?”
Pia aliwataka mawaziri wa Wizara za Viwanda na Biashara kutoka pande zote za Muungano wahakikishe kwamba bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya hapa nchini na zile zinazoingizwa kutoka nje, zinakuwa na maelezo ya Kiswahili ili kuwapa fursa watumiaji wazitumie wakiwa wanafahamu vema maelekezo yaliyomo kwenye bidhaa hizo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema lugha si maneno tu yanayozungumzwa mtaani na ofisini, bali ni maisha ya watu na ndiyo yenye kurahisisha mawasiliano katika shughuli za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
“Katika muktadha wa utangazaji kwenye vyombo vya habari, hakuna lugha duniani inayosimama peke yake. Kwa msingi huo, ndoto ya kuifanya lugha ya Kiswahili izungumzwe duniani kote ni matarajio ya kila mmoja wetu. Hatua iliyofikiwa sasa ni nzuri kwani kinafundishwa kwenye vyuo vikuu vya nje vingi na sasa Kiswahili kinatumika kwenye vyombo vya habari kama radio kwenye nchi mbalimbali na tunatarajia kupitia kusambaa huku tutaandika vitabu vingi ili kupata watu wengi zaidi,” alisema.
Alisema moja ya mkakati unaofanywa na Serikali kwa sasa ni kuwaagiza mabalozi wa Tanzania walioko nje ya nchi waanzishe madarasa ya Kiswahili kama njia ya kukikuza na kukitangaza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Bi. Tabia Maulid Mwita alisema zipo idhaa nyingi zinazotumia Kiswahiliambapo baadhi ya nchi zilianza kutangaza kwa Kiswahili yapata miaka 66 sasa.
Alisema wizara yake itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika nyanja zote huku akisisitiza msemo wa “tumia chako mpaka usahau cha mwezako.”
Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) lilikuwa na kaulimbiu isemayo: “Kiswahili ni nyenzo ya mawasiliano, tujiamini kukitumia” na lilishirikisha wadau kutoka Tanzania, Kenya, Ethiopia, Burundi, Rwanda na Tehran. Taasisi zilizoshiriki ni BAKITA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, VOA, UN-NEWS (Kiswahili), Radio Tehran, Radio Maria, Radio Karagwe, ZBC, TBC, BBC, KBC, ITV, UFM, UTV na Ngassa FM.