Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wauguzi 15 kutoka hospitali mbalimbali nchini walioshiriki mafunzo ya wiki 30 ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakati wa hafla fupi ya kuhitimu mafunzo hayo iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam
Wauguzi kutoka Hospitali mbalimbali nchini walioshiriki mafunzo ya wiki 30 ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakisikiliza wakati wa hafla fupi ya kuhitimu mafunzo hayo iliyofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliyopo jijini Dar es Salaam
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi Joshua Ogutu akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo wakati wa hafla fupi ya kuhitimu iliyofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpa cheti mhitimu wa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi mshiriki wa mafunzo hayo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya wiki 30 ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wahitimu hao iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Na: Mwandishi Maalum
Wahitimu wa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wametakiwa kuwa na upendo na kuwajali wagonjwa hao pindi wanapokuwa wanawahudumia kwa sababu wagonjwa hao wanahitaji upendo wa hali ya juu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokuwa katika hafla fupi ya kuwapongeza wahitimu hao iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema wahitimu hao wamejifunza namna ya kuwahudumia wagonjwa mahututi kwa muda wa wiki 30 hivyo wanatakiwa kwenda kufanya vizuri zaidi ya walivyokuwa wakifanya hapo awali kabla ya kujifunza mafunzo hayo.
“Wagonjwa mahututi wanahitaji huduma ya karibu, hivyo mnapaswa kuwahudumia kwa kuwaonyesha upendo na kuwajali kwani kwa kufanya hivyo mtawapa faraja na watapona haraka, pia mfahamu ya kwamba sisi sote ni wagonjwa wa kesho hivyo basi tuwahudumie wenzetu vizuri ili na sisi tutakapokuwa wagonjwa tuhudumiwe inavyostahili”, alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt Kisenge alisema Serikali imeongeza vyumba vya wagonjwa mahututi katika hospitali za kanda hivyo kuongeza uhitaji wa wauguzi wa wagonjwa mahututi na kuwataka wahitimu hao kutumia fursa hiyo kwenda kuziba mapengo hayo na kuonyesha ujuzi walioupata kwa ubora na ustadi wa hali ya juu.
“Huko mnakoenda kwenye vituo vyenu vya kazi mnatakiwa muwe mfano wa kuigwa kwa kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi vizuri na pia kuwafundisha wengine namna ya kuwahudumia wagonjwa hao kwa kuwajali na kuwathamini”, alisisitiza Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uuguzi JKCI Salma Wibonela alisema kupitia mafunzo hayo wahitimu hao wanaenda kuwa mabalozi wazuri kuwahimiza wauguzi wenzao kupata mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi.
“Kupitia mafunzo haya mkaeneze ujuzi huu kwa wengine ili nao waweze kupata mafunzo haya kwani wauguzi wote mkipata mafunzo haya wagonjwa watapata huduma inayostahili”, alisema Salma
Naye mhitimu wa mafunzo hayo Cecilia Luoga alisema wamejifunza namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi, kutumia vifaa tiba kama vile kifaa cha kupima ufanyajikazi wa moyo (Ventilator) pamoja na kumhudumia mtu aliyepata shambulio la moyo kwa ghafla (Advance Cardiovascular heart Attack).
“Katika mafunzo haya tumejifunza kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura kwa kuwajali na kuwaonyesha tumaini kuwa huduma wanayoipata inaenda kuondoa changamoto walizokuwa nazo”, alisema Cecilia
Akiushukuru uongozi wa JKCI Cecilia alisema Uongozi huo uendelee kutoa mafunzo hayo kwa wataalam wa afya nchini kwani uhitaji wa elimu hiyo ni mkubwa.
“Tunaishukuru sana JKCI kwa jitihada zote mlizozifanya kutupa mafunzo haya mzuri ya kuokoa maisha ya wagonjwa wahututi na wanaohitaji huduma ya dharura, tuanaahidi yote mliyotufundisha tutayafanyia kazi , alisema Cecilia