Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa tamasha la Pasaka kila mwaka Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu uwepo wa Tamasha la Pasaka litakalofanyika bure bila kiingilio april 9,2023 katika Viwanja vya Leders Club Jijini Dar es salaam.
Mratibu wa Tamasha la Pasaka Bw. Emmanuel Mabupa (kushoto) akifafanua jambo kuhusu maandalizi ya Tamasha hilo.
Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Upendo Nkone akizungumzia jinsi alivyojipanga kushiriki kwenye Tamasha la Pasaka litakalofanyika April 9,2023 katika Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam.
Emmanuel Zabron kutoka katika kundi la Zabron Singers akiiimba wimbo wao maarufu wa ‘Nimeuona Bwana Mkono wako Bwana’ mbele ya waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa tamasha la Pasaka kila mwaka Alex Msama amesema kuwa tamasha hilo mwaka huu litafanyika katika viwanja vya Leaders Club vilivyopo kinondoni Jijini Dar es Salaam na kwamba hakutakuwa na kiingilio.
Msama ameyasema hayo leo Machi 19,2023 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Ofisi za Kampuni hiyo ilizopo kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa waimbaji mbalimbali kutoka Tanzania na nchi za Afrika Mashariki watatumbuiza.
“Maandalizi ya tamasha la Pasaka yanaendelea vizuri, hapo awali tamasha letu lilitakiwa lifanyike uwanja wa Taifa, lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu tamasha hili halitafanyika tena Uwanja wa Uhuru na badala yake litafanyika katika viwanja vya Leaders club kwa hiyo tamasha lipo kama kawaida tarehe 9 mwezi April, na mpaka sasa waimbaji wengi wamethibitsha kushiriki” amesema Msama.
Aidha amesema kuwa Tamasha hilo pia litakuwa la kumshukuru Mungu katika kusherehekea miaka miwili ya uongozi wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba watatumia nafasi hiyo kumuombea ili aendelee kuiongoza nchi ya Tanzania kwa amani.
“Tamasha letu pia ni la kumshuru Mungu kwaajili ya uongozi wa mama yetu , Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili madarakani kwa mafanikio makubwa, miradi mingi imeendelea, kila kitu kinaenda vizuri, tunaishi kwa amani na utulivu hivyo ni lazima tumshukru Mungu kwa uongozi wa Rais wetu” ameongeza Msama.
Kwa upande wao baadhi ya waimbaji watakaoshiriki kwenye Tamasha hilo, Upendo Nkone na Emmanuel Zabron kutoka katika kundi la Zabron Singers, kwa nyakati tofauti wametoa mwito kwa wananchi hususani wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye Tamasha hiyo huku wakiahidi kukonga nyoyo wananchi hao kwa kutoa burudani safi.
Naye mratibu wa Tamasha la Pasaka Bw. Emmanuel Mabupa amesema kuwa mpaka sasa waimbaji wote walioalikwa kushiriki kwenye Tamasha hilo wamethibitisha ushiriki wao na kwamba maandalizi yote yanaenda vizuri.
“Hayawi hayawi sasa yamekuwa, lile tamasha lililokuwa likisubiriwa kwa miaka mingi la Pasaka sasa kufanyika katika viwanja vya Leaders Club bure bila kiingilio, hivyo wananchi wasisite kutoka na familia zao kuhudhuria kwenye tamamsha hilo” amesema Mabupa.