******************
Na John Walter-Manyara
Katika Mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023-2024 katika mkoa wa Manyara, wizara ya fedha na mipango imekadiria ukomo wa bajeti wa jumla ya shilingi bilioni 255,554,40,041 ambapo kati ya fedha hizo ruzuku ya matumizi ya kawaida ni bilioni 184 na ruzuku ya maendeleo ni bilioni 70.
Akiwasilisha mpango huo katika baraza la ushauri la mkoa mbele ya mwenyekiti wa baraza, mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere, Katibu tawala msaidizi mpango na uratibu Maarufu Mkwaya amesema kwa upande wa maendelo kuna vipengele vitatu ambavyo ni pesa za ndani kutoka makusanyo ya TRA ambapo wanatarajia kukusanya bilioni 39.813, fedha za nje kutoka kwa wadau na wahisani shilingi bilioni 24.946 huku wakitajia kutenga shilingi asilimia 40 ya maendeleo kutoka halmashauri shilingi bilioni 6.53.
Shughuli za maendeleo kwa upande wa Halamashauri za mkoa wa Manyara ambazo zinatarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kujenga majengo ya utawala, kununua thamani katika jingo la halmashauri ya Babati, Mbulu mji ambapo tayari wametengewa bilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi japo pesa bado hawajapokea, ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali, zahanati na vituo vya afya, ujenzi wa nyumba za watumishi (WAKUU WA IDARA), ujenzi wa vituo vya afya.
Katika ngazi ya mkoa, zimetengwa shilingi Bilini 1.2 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa ofisi za wakuu wa wilaya kwenye wilaya za Babati na Kiteto ambapo kwa mwaka 2023 bajeti iliyopo ni shilingi Milioni 875 kwa hizo ofisi mbili kwa kila moja ambapo ujenzi umeanza kwa hatua ya awali ofisi ya Mkuu wa wilaya Babati huku kiteto wakiwa kwenye hatua za manunuzi.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa mkoa una mpango wa kukamilisha nyumba za makatibu tawala wa wilaya za Simanjiro na Mbulu pamoja na kukamilisha nyumba ya makazi ya mkuu wa wilaya Hanang’ ambapo jingo hilo kwa sasa linawekewa Tiles.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amewataka wakurugenzi, wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri, vijiji, watendaji wa vijiji na mitaa kushirikiana katika makusanyo ya ndani ili malengo yaliyowekwa yatimie.