Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu maendeleo ya Utekelezaji wa mradi wa barabara za mwendo kazi awamu ya pili eneo la Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Mbunge wa Kyela na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na, Mhe Ally Kinanasi akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi(hawapo pichani), wakati kamati hiyo ilipotembela mradi wa barabara za mwendo kazi awamu ya pili eneo la Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya mwendo kasi awamu ya pili inayoshia Mbagala.
Mbunge wa Kilombero na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na, Mhe. Aboubakari Asenga akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi(hawapo pichani), wakati kamati hiyo ilipotembela mradi wa barabara za mwendo kazi awamu ya pili eneo la Mbagala, jijini Dar es Salaam
PICHA NA WUU
**********************
Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha wanaingia mikataba ya ujenzi yenye gharama isiyokuwa na nyongeza za fedha.
Imesema wakandarasi wengi wanaoingia mikataba ya ujenzi na Tanroads wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayoisababishia serikali gharama zisizokuwa na tija.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Dart awamu ya pili eneo la Mbagala.
“Serikali imetoa fedha nyingi katika ujenzi wa mradi huu. Jitihada ni nzuri zimefanyika, tumeridhika na kwa sasa kuna maendeleo. Lakini igeni mfumo wa TRC katika ujenzi wa barabara. Wakandarasi wanakuja na mfumo wa nyongeza za gharama hali inayosababisha miradi kuwa na gharama kubwa,” alisema Kakoso.
Mbali na kutoa agizo hilo, kamati hiyo iliagiza Tanroads wanapojenga Miundombinu wazingatie uelekeo ya maji kutotiririka kuelekea kwa wananchi.
Pia Tanroads wanapaswa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya chini ya madaraja pamoja na mikataba wanayoingia imalizike kwa wakati na kusiwepo na nyongeza ya muda.
Kadhalika, kamati hiyo ilitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi ya serikali ili kuleta maendeleo endelevu.
Akizungumza baada ya maagizo hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema wameyapokea maagizo hayo na watayafanyia kazi.
Profesa Mbarawa alisema kuhusu mfumo wa nyongeza ya gharama kwa wakandarasi watakwenda kujifunza kwa TRC.
Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila akiwasilisha taarifa ya mradi huo alisema ujenzi hadi sasa umefikia asilimia 89.9 na ulipaswa kukamilika Machi 27, mwaka huu lakini mkandarasi ameomba nyongeza ya muda ya miezi saba zaidi ili akamilishe.
Alisema baada ya kumpokea maombi hayo wanaendelea kuyafanuyia kazi kuhusu uhalaki wake.
“Tathmini iliyofanywa inaonyesha kuwa gharama ya mkataba itaongezeka kutoka Sh. 217.48 bilionii hadi Sh. 253.91 ongezeko hili la asilimia 56.7″alieleza Mativila.
Alisema sababu nyingine ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbalimbali zaidi ya makisio ya awali ni maboresho ya usanifu.
“Daraja la Kigogo kuvuka Mto Msimbazi kwenye Barabara ya Kawawa pia halitaweza kujengwa kupitia kandarasi hii kutokana na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa haraka awamu ya pili,” alisema Mativila.
Alibainisha kuwa ujenzi wa daraja hilo haukuwa sehemu ya kazi zilizokusudiwa kufanywa toka awali.