Na Mwandishi wetu, Arusha
IKIWA Machi 21 kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya ulemavu wa akili au ubongo aina ya Down Syndrome, unaoathiri uwezo wa watoto kujifunza na hata muonekano wa maumbile, jamii imetakiwa kuacha kuwaficha watoto wenye tatizo hilo kwa kuwa wana haki sawa na watoto wengine.
Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanafanyika jijini Arusha na yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Taasis ya PPDSF (Down Syndrome Tanzania) inayozungumzia watu wenye ‘Down Syndrome’.
Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Mwenyekiti Mwanzilishi wa Taasisi hiyo, Mony Teri Pettit, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa watoto wenye tatizo hilo wana haki zote kama binadamu wengine hivyo wasifichwe.
“Watu wasiwafiche watoto wao wana haki kama watu wengine kwa namna nyingine jamii inapaswa kuwakubali na kuwapa haki zote stahiki,” alisema.
Aidha alisisitiza utambuzi wa watoto wa aina hiyo ufanyike pindi wanapozaliwa.
“Tunaomba utambuzi uwe wa mapema pindi wanapozaliwa kuwe na ustawi wa jamii wa kufuatilia kwani asilimia kubwa ya hawa watoto wanakuwa na magonjwa ya moyo yanayopelekea kufariki wakiwa na umri mdogo,” alisema.
Alisema maadhimisho hayo yanalenga kupaza sauti katika kujenga ufahamu kwa jamii juu ya hali ya ‘Down Syndrome’ ili wafikie malengo yao.