WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk, Seleman Jafo amezindua kampeni ya ‘Play 2 ziro’ inayolenga upandaji miti kwa shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 18, 2023 katika shule ya Sekondari Minaki wilayani Kisarawe mkoani Pwani, ambapo miche 200 ya mipera imepandwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Jaffo amesema mabadiliko ya tabianchi sio ya kusimuliwa kwani yapo dhahiri Tarangire, Manyara wanyama wanafariki kutokana na ukame kwa kukosa maji na malisho, wilayani Longido na maeneo mengine ya nchi hali ni mbaya.
“Tukumbuke nchi yetu inapitia katika kiangazi kikubwa sana, kidogo baadhi ya mikoa siku mbili hizi mvua imenyesha lakini kwa uchache sana, maji kukauka hata katika Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya mikoa mingine Tanzania, hali ni mbaya,” amesema Jaffo na kuongeza:
“Kampeni hii serikali inaipa kipaumbele kwa sababu inatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu, ambaye ni ajenda ya kutunza mazingira,” amesema.
Amesema ajenda hiyo inachangisha ajenda ya maendeleo ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira na kuwafanya wanafunzi kuwa na utamaduni wa kupanda miti kuanzia wakiwa wadogo, lengo ikiwa ni kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kuyahifadhi mazingira.
Katika kampeni hiyo ya ‘Play 2 Ziro’ inayofanywa na taasisi ya African Lyon Foundation inalenga kupanda miti ya matunda 1600 katika shule nane, ambapo kila shule itapanda miti 200.
Akizungumzia hilo Jaffo amesema: “Maana yake katika miti 200 kuna mingine ambayo inaweza isistawi vizuri au ikaishia njiani, lakini tunatarajia miti 800 iwe imestawi vizuri, walimu ninawaagiza muhakikishe miti inastawi katika shule zenu.
“Shule zitakazofanya vizuri zitapata bonasi. Kuna kitengo cha ufuatiliaji na tathmini kikibaini shule fulani imefanya vizuri miti yao imestawi vizuri, lazima ipewe bonasi, nawaomba walimu msimamie vyema programu hii ya play 2 ziro,” amesisitiza.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Afrian Lyon Foundation, Rahim Kangezi, ameishukuru serikali kuunga mkono kampeni hiyo ambayo inalenga kuwekeza katika jamii.
Kangezi alimkabidhi Waziri Jaffo ripoti mbili ambazo wameziandaa ikiwemo ya kampeni ya linda tembo wetu na ya chanjo ya uviko 19.
Naye, Ofisa Maliasili kutoka Mkoa wa Manyara, Michael Gwadu amesema, mradi wa Play 2 Ziro ambao unajihusisha na michezo na uhifadhi wa mazingira, una lengo la kupunguza gesi joto kufikia ziro, hivyo wanafunzi watacheza na hapo hapo kulinda mazingira.
Amesema mradi huo awamu ya kwanza unatekelezwa katika mikoa nane, ambayo ni Tabora, Pwani, Morogoro, Lindi, Tanga, Manyara, Singida, Dodoma na Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, African Lyon Foundation imeahidi kujenga ‘Computer Lab’ katika shule ya Minaki pamoja na kuwawekea vifaa vya kisasa ili watunze mazingira kidigitali.
Pia wametoa mipira 10 kwa kila shule ambazo zinapitiwa na mradi huo. Tayari shule za |Chanzige A na B, Sanza, Kibasila na Minaki zimenufaika.