Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwasilisha vipaumbele vya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa wakuu wa wilaya ili kuwajengea uelewa utakaowasaidia kusimamia utekelezaji wa vipaumbele vinavyotekelezwa katika maeneo yao ya utawala, wakati wa kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika jijini Dodoma
Sehemu ya wakuu wa wilaya nchini wakiwa katika kikao kazi cha kusikiliza vipaumbele vya wizara mbalimbali vipaumbele vinavyotekelezwa katika maeneo yao ya utawala, wakati wa kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wakuu wa wilaya wote nchini kuweka ajenda ya mazingira kama kipaumbele katika maeneo yao.
Pia, amewataka wakuu hao wa wilaya kubuni mikakati endelevu ya kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ili kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kupata nishati hiyo ya kupikia iweze kupungua.
Ametoa wito huo Machi 17, 2023 wakati akiwasilisha vipaumbele vya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa wakuu wa wilaya ili kuwajengea uelewa utakaowasaidia kusimamia utekelezaji wa vipaumbele vinavyotekelezwa katika maeneo yao ya utawala.
Akiendelea kuzungumza wakati wa semina elekezi iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na kufanyika jijini Dodoma, Waziri Jafo ametoa wito kwa wakuu wa wilaya kuendelea kusimamia vyema zoezi la upandaji wa miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri.
Aidha, Dkt. Jafo amewapongeza viongozi hao kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha kuwa mazingira yanahifadhiwa kwa maendelevu kwa kusimamia vyema zoezi la upandaji miti.
“Ndugu zangu tangu tuzindue Kampeni Kabambe ya Hifaddi na Usafi wa Mazingira tarehe tano mwezi wa sita mwaka 2021, ninyi wakuu wa wilaya mmekuwa mkisimamia ipasavyo kampeni hii kwa kuhamasisha upandaji wa miti, mmemuheshimisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Pamoja na hayo pia Waziri Jafo amewasihi wakuu wa wilaya kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuepuka changamoto ya kukauka kwa vyanzo hivyo hali inayoweza kusababisha uhaba wa maji kama ambavyo uliikumba nchi yetu katika baadhi ya maeneo hivi karibuni.
Hatua ya wizara kuwasilisha vipaumbele hivyo ni kunatokana na maombi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ya kutaka wakuu hao kupitishwa kwenye utekelezaji wa shughuli za wizara za kisekta ili kwenda kusimamia na kutekeleza majukumu hayo kwa weledi.
Lengo la uwezeshaji huo katika kuwajengea uwezo Wakuu wa Wilaya ili kuwawezesha kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa weledi na kuelewa mipaka na miongozo ya kusimamia wakati wanatekeleza majukumu yao.