Na. Damian Kunambi, Njombe
Wafanyabiashara wa nyama ya Nguruwe (Kitimoto) Wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuhakikisha wanasimamia kikamilifu katazo walilolitoa juu ya uuzaji na ulaji wa nyama ya Nguruwe ili kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Nguruwe unamalizika mapema na kurejea taratibu za kawaida kama ilivyo zoeleka.
Hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Dkt. wa mifugo wa halmashauri hiyo ya Ludewa Festo Mkomba kutoa tangazo la kuzuia uuzaji na ulaji wa nyama hiyo kutokana na kubainika kwa uwepo wa ugonjwa wa homa ya Nguruwe katika halmashauri hiyo ambapo mpaka sasa umebainika kuwepo katika kata ya Mawengi na Lugarawa.
Hata hivyo wafanyabiashara wa nyama hiyo ya Nguruwe wameonyesha hofu ya kupoteza mitaji yao huku mmoja wao aliyetambulika kwa jina la Edward Shagama ameiomba serikali kusimamia vyema zuio hilo kwani linapotokea janga kama hili baadhi ya watu huchinja Nguruwe wao wakiepuka kupata hasara na kutembeza mitaani wakitangaza kuwa wanauza mchicha ili isiweze kujulikana.
“Mimi naiomba serikali iweke ulinzi wa kutosha ili kusije tokea watu mitaani wanaichinja nguruwe na kutembeza kwenye majumba ya watu kwa kutangaza kuwa wanauza mchicha na kumbe wanauza nyama za nguruwe halafu matokeo yake ugonjwa ukazidi kuenea na sisi tukacheleweshwa kuendelea na biashara zetu mwishowe tutakula mitaji” Amesema Shagama.
Aidha kwa upande wake Daktari wa mifugo wa Halmashauri hiyo Festo Mkomba amewaomba wananchi kuonyesha ushirikiano wao katika hili ili kutokomeza ugonjwa huo kwa haraka kwani endapo kutafanyika uuzwaji huo kwa njia za kificho kutapelekea ugonjwa kuendelea kuenea na kuuwa Nguruwe wengi zaidi.
Amesema katika suala la ulinzi tayari kamati ya ulinzi na usalama kuanzia ngazi za kijiji tayari zimekwisha anza kazi na hata katika idara ya Mifugo inatarajia kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya wilayani hiyo ili kutoa elimu ya ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa ugonjwa huo mpaka sasa haujabainika kuwa na madhara yeyote kwa binadamu isipokuwa kwa nguruwe pekee hivyo wanaweka zuio la ulaji kwakuwa njia mojawapo ya kuenea kwa ugonjwa huo husababisha na binadamu.
“Binadamu ni chanzo mojawapo cha kueneza ugonjwa huu, anapokula nyama ya Nguruwe aliyekuwa na ugonjwa halafu akaenda kumgusa Nguruwe aliye mzima au yale masalia ya nyama aliyokula akiweka jirani na Nguruwe aliye mzima basi Nguruwe huyo atakuwa tayari amekwisha ambukizwa ugonjwa huo”.
Aidha ameongeza kuwa wanafanya jitihada za kutokomeza ugonjwa huo kwani kwa wilaya hiyo ya Ludewa hutegemea zaidi kitowewo cha nyama ya Nguruwe ukilinganisha na ng’ombe ambapo takwimu huonyesha kuwa kwa siku huliwa nyama ya Nguruwe zaidi ya kilo 10,000 huku nyama ya ng’ombe ikiliwa kwa zaidi ya kilo 5,000 pekee.