Muonekano wa Barabara ya Hinga-Litolomelo iliyofanyiwa matengezo yenye jurefu wa kilomita 11.7 iliyofanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe na wakala wa Barabara za vijijini na mijini Tarura wilayani Nyasa ambayo kwa sasa imewezesha kufungua mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya kata ya Ngumbo wilayani Nyasa.
Na Muhidin Amri,
Nyasa
BAADHI ya wananchi wa kata ya Ngumbo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameishukuru serikali kwa kuifungua barabara ya Hinga-Litolomelo na Ngumbo-Litoho zinazounganisha wilaya ya Mbinga na Nyasa na maeneo mengine mkoani humo ambazo awali zilikuwa hazipitiki kirahisi.
Wamesema,kufunguka kwa barabara hizo katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kumerahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo na samaki na kumaliza kero ya usafiri iliyokuwepo kwa muda mrefu.
Wamesema,changamoto kubwa kwa wananchi wa kata ya Ngumbo ilikuwa barabara za kuunganisha kata hiyo na maeneo mengine,lakini sasa kero hiyo haipo baada serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura) kutoboa na kufanya matengenezo ya makubwa ya barabara hizo kwa kiwango cha changarawe.
John Mkomola mkazi wa kijiji cha Ngumbo amesema,serikali ya awamu ya sita imewatendea haki kwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo barabara zinazokwenda kuchochea na kuharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema,baadhi ya maeneo katika wilaya ya Nyasa hayakuweza kufikiwa na baadhi ya huduma za kijamii kwa kukosa barabara, hivyo kusababisha maisha ya wananchi kuwa magumu licha ya wilaya hiyo kuwa na rasimilia kubwa ya ardhi na ziwa Nyasa lenye samaki wengi.
Adolat Kapinga mkazi wa kijiji cha Lugali amesema,awali barabara ya Ngumbo-Litoho inayounganisha wilaya ya Nyasa na Mbinga haikuweza kupitika kwa urahisi kutokana na ubovu hasa mashimo makubwa na wakati wa masika kuwa na utelezi na hivyo kusababisha magari kukwama na hata kulala barabarani.
Aidha ameeleza kuwa,katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia barabara hiyo imeimarika na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hizo mbili ambao sasa wanatembea kifua mbele na kufaidi matunda ya serikali yao.
Kapinga ameipongeza wakala wa barabara za vijijini na mijini Tarura wilayani Nyasa kufanya matengenezo ya barabara na kurudisha mawasiliano katika maeneo mengi ya wilaya hiyo ambayo hapo awali hayakufikika kwa urahisi.
“miaka miwili ya Rais Dkt Samia tunaona mabadiliko mengi na makubwa katika wilaya yetu,barabara hii haikuweza kupitika kirahisi, lakini sasa serikali imefanikiwa kuunganisha mawasiliano kati ya wilaya ya Mbinga na Nyasa”amesema Kapinga.
Kwa upande wake meneja wa Tarura wilaya ya Nyasa Thomas Kitusi alisema,barabara ya Hinga-Litolomelo ni moja ya barabara saba zilizotengenezwa kwa fedha za tozo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yenye urefu kilomita 11.7 kwa gharama ya shilingi milioni 174 kwa kiwango cha changarawe.
Kitusi alitaja barabara nyingine ni Ngumbo –Litoho yenye urefu wa km 6.59 ambayo ilitengewa jumla ya shilingi milioni 84 kwa ajili ya kufanya matengenezo kwa kiwango cha chanagarawe.
Alisema,katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya barabara ikilinganisha na miaka ya nyuma. na ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha nyingi ambazo zimewezesha Tarura kufanya matengenezo ya barabara nyingi za vijijini zilizoleta mabadiliko makubwa.