Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imezuia kufanyika kwa Mkutano wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) uliopangwa kufanyika kesho Machi 17,2023 Jijini Tanga ili kujaza nafasi za Makamu wa Rais na Mhazini Mkuu wa chama hicho baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Deus Seif na Mhazini Mkuu Allawi Abubakari kupinga kutimuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Wakili wa upande wa waleta maombi Nashon Nkungu baada ya kutolewa maamuzi hayo na Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Dodoma Gerson Mdemu wa divisheni ya kazi amesema uamuzi huo unatoa nafasi kusikilizwa kwa kesi ya msingi ya waleta maombi ya kuitaka Mahakama Kuu kutoa tafsiri ya mkutano mkuu wa nusu mwaka kuwajadili waleta maombi wakati wakisubiri hukumu ya kesi ya jinai mahakama kuu.
Amesema sababu iliyosababisha waleta maombi waombe zuio la mahakama na kupewa ni uwepo wa kesi ya kujadili uhalali wa wao kuondolewa kama wanachama na kuondolewa kwenye nafasi za uongozi walizokuwa wakizitumikia.
Hata hivyo, mwezi Desemba mwaka jana, Mkutano mkuu wa nusu muhula wa CWT, uliazimia kuwafuta uanachama Seif na Allawi kutokana kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na Mahakama ya Kisutu baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha Sh. Milioni 13.9 ambazo ni mali ya CWT na hivyo kukosa sifa ya kuwa viongozi na wanachama
Mkutano mkuu wa chama cha walimu cwt ulipangwa kufanyika kesho Machi 16,2023 jijini Tanga huku baadhi ya wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini wakianza kuwasili.