Na John Mapepele
Shamrashamra za hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro zimepambamoto katika Makao Makuu ya Hifadhi hii Mkoani Kilimanjaro.
Maadhimisho haya yanafanyika leo Machi 16, 2023 ambapo Mgeni Rasmi ni Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii Mhe Mohamed Mchengerwa.
Katika hafla hii Mhe. Mchengerwa anatarajia kutoa Tuzo kadhaa kutambua mchango wa watu mbalimbali walioutoa katika Hifadhi hii maarufu duniani.
Miongoni mwa watu watakaokabidhiwa Tuzo hizo ni pamoja na familia ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Aidha, Mhe. Mchengerwa atashuhudia tukio la kusaini mkataba wa kusaidia uhifadhi katika Hifadhi hii kutoka Serikali ya China.
Kwa upande wa Tanzania Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Anderson Mutatembwa atawakilisha wakati kwa upande wa Kenya, Mhe. Balozi wa China nchini atasaini mkataba huo.
Pia Mhe Mchengerwa anatarajiwa kukabidhiwa mfano wa Hundi ya Dola za kimarekani milioni moja kutoka Serikali ya China kama msaada kwa Hifadhi ya Kilimanjaro.
Hifadhi hii ni ya pili kwa makusanyo ikiongizwa na Serengeti kwa Hifadhi zinazosimamiwa na Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA).
Kwa mwaka wa fedha 2021/22 ilikusanya bilioni 581.8 kutoka kwa watalii 467,190 waliotembelea Hifadhi hiyo.
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ilianzishwa rasmi Machi 16, 1973 na ni miongoni mwa Hifadhi maarufu duniani.