RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (kulia), akifungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa maabara nne mpya za Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), uliofanyika Machi 15, 2023.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwa na viongozi wengine wa serikali, akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa maabara za Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) uliofanyika Machi 15, 2023.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (kushoto), akipokea zawadi maalumu ya kutambua mchango wake katika masuala ya viwango toka kwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, wakati wa hafla ya uzinduzi wa maabara za Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) uliofanyika Machi 15, 2023.
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) (ZBS), Yussuph Majid Nassor (kulia), akitoa maelelezo kuhusu mja ya maabara nne zilizozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipokua akizikagua maabara hizo kabla ya kuzizindua.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akihutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa Maabara nne mpya za (ZBS), uliofanyika Machi 15, 2023 huko Maruhubi nje kidogo ya mjii wa Zanzibar.
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali ina nia ya dhati kuona wananchi wanaendelea kutumia bidhaa zenye viwango, usalama na ubora unaostahiki.
Dk. Mwinyi alieleza hayo alipokua akihutubia wananchi baada ya kuzindua maabara nne mpya za Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Maruhubi, wilaya ya Mjini Zanzibar.
Alisema serikali imekua ikichukua hatua stahiki kupima ubora wa bidhaa zinazoingizwa au kuzalishwa nchini ili zisilete madhara kwa watumiaji na mazingira.
Aidha Dk. Mwinyi alisema kupitia ZBS, serikali imekua ikilifanyia kazi suala la mpango wa usalama wa afya za wananchi kwa vitendo katika kuimarisha maabara za uchunguzi kulingana na mahitaji.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha inajenga uwezo wa ukaguzi wa bidhaa mbali mbali zinazozalishwa nchini na zile zinazoingiwa kutoka nje ili ziweze kukidhi vigezo kulingana na viwango vya kimataifa”, alieeleza Dk. Mwinyi.
Alibainisha kuwa anaridhishwa na hatua zinqazochukuliwa na taasisi hiyo za kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini kwa ajili ya kukuza uchumi na kuimarisha hali za kiafya za wananchi wetu.
Aliongeza kuwa kutokana na hatua hizo, jami inaepushwa na hatari za kiafya zinazoweza kuwakabili wananchi kwa kuwepo wafanyabiashara wasiokua waadilifu wanapoingiza bidhaa zisizokua na ubora au zilizopitwa na muda wa matumizi.
“Kwa hatua hii, tunafungua ukurasa mpya wa maendeleo katika suala la uchunguzi wa ubora wa bidhaa hapa Zanzibar, kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa,” alisema.
Alisema sera ya biashara huria iliyoanza kutekelezwa katika miaka ya 80 iliwapa nafasi wafanyabiashara binafsi kuleta bidhaa Zanzibar kutoka maeneo mbali mbali duniani.
Akizungumzia uwepo wa taasisi hiyo, Dk. Mwinyi alisema Baraza la Wawakilishi lilitunga sheria ya Viwango ya Zanzibar namba 1/2011 ambapo kupitia sheria hiyo ZBS ilipewa jukumu la kuweka viwango na kusimamia ubora wa bidhaa na huduma mwaka 2012 ilipoanzishwa.
“Jukumu kubwa la taasisi hii ni kuhakikisha kuwa soko la Zanzibar linakuwa na bidhaa zenye ubora unaostahili na ni matumaini yangu uwezo wa maabara hizi utapelekea kupatikana kwa ufanisi na wa haraka katika kupata majibu ya sampuli za bidhaa zinazoingizwa au zinazozalishwa”, aliongeza Dk. Mwinyi.
Aliwakumbusha watendaji wa ZBS kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, uaminifu na kujiamini na kuzingatia kuwa kazi yao ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda, wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema malengo ya serikali ni kuona nchi inakuwa na bidhaa zenye viwango hivyo uwepo wa maabara hizo kunaongeza uwezo wa taasisi kutekeleza majukumu yake.
Alieleza kuwa uzinduzi wa maabara hizo kunaifanya ZBS kuwa na maabara saba kutoka tatu zilizokuwepo awali na kueleza kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
“Katika kipindi cha miaka miwili toka niwe waziri, nimeshatangaza viwango vya bidhaa na huduma mbali mbali 227, kiwango ambacho ni kikubwa ambayo ni mafanikio makubwa kwa wizara yetu na ZBS”, alieleza Omar.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa tasisi hiyo, Yussuph Majid Nassor, alisema ili kufanyika ukaguzi wa bidhaa na vifaa vitakavyokidhi mahitahi suala la maabara za kisasa zina nafasi kubwa hivyo watahakikisha wanaongeza ufanisi kwa kuwepo maabara zenye viwango.
Alisema uzinduzi huo unahusisha maabara ya kemia ya chakula iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 300, maabara ya vifungashio iliyogharimu zaidi ya bilioni 2, maabara ya upimaji wa bidhaa iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 na maabara ya umeme iliyogharimu shilingi milioni 275.
Yussuph alisema kuwa taasisi hiyo imepiga hatua ikiwemo ujenzi wa maabara ya vifaa vya ujenzi kwa ufadhili wa World Bank kupitia mradi wa BIG-Z ambayo itakuwa na uwezo wa kupima vifaa vyote vya ujenzi Zikiwemo nondo, matofali, saruji na vifaa nyengine ambapo ujenzi utakaogharimu shilingi bilioni mbili.
“Pia hivi karibuni tunatarajia kuanza ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa upimaji wa magari ambacho kitakuwa na uwezo wa kukagua magari 150 kwa siku,” alisema Yussuph.
Aidha aliahidi kwamba ZBS itaendelea kusimamia ubora wa bidhaa na huduma kwa kupata vifaa vipya katika maabara zake zitakazopelekea upimaji wa bidhaa nyingi zaidi ikiwemo za chakula.