**************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Machi 15
Abdallah Salum (Dulla Mchoraji),mkazi wa Mailmoja Kibaha, Mkoani Pwani anadaiwa kutaka kumuingilia(KUBAKA) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule moja ya msingi iliyopo Mjini Kibaha.
Dulla anadaiwa kufanya tukio hilo ikiwa ni mara ya pili kwa mtoto huyo Hali iliyosababisha wananchi wenye hasira Kali kumpa kichapo na kufikishwa polisi kwa hatua zaidi za kiuchunguzi ili sheria ichukue mkondo wake.
Akihojiwa kutokana na tukio hilo ,ambalo linadaiwa kufanyika Machi 13 kwenye vichaka karibu na eneo la Garden Mailmoja, Kamanda wa polisi mkoani Pwani Pius Lutumo ,alikiri kupata taarifa na kusema ni shambulio la aibu na sio kosa la Ubakaji.
Alieleza ,kwa taratibu za Jeshi la polisi , taarifa zao zinakamilika baada ya uchunguzi wa kina na hawabishani na taarifa za jamii bali kwa kielelezo Cha uchunguzi.
“Nilikuwa nikifuatilia tukio hili mara uliponipigia kunihoji Mwandishi,ila tukio hili inasemekana liliripotiwa kituo Cha polisi kwa madai ya Dulla kumuingilia mtoto huyo kwa mara ya kwanza miezi kadhaa iliyopita,na alipopelekwa hospital aligundulika hakuwa na michubuko Wala hajaonekana kuingiliwa “
“Hili ni tukio la mtu huyu mmoja kuhusika Tena kumbaka huyu mtoto Lakini kwa Mazingira yale yale ya kiuchunguzi inaonekana kwa taarifa za hospital hajaingiliwa ,ni mfanano wa shtaka la kwanza”
“Kwa maelezo ya huyu mtuhumiwa anadai yeye ni Mchoraji, wanafunzi huwa wakienda kushangaa shangaa tu wakati akichora na huyu mtoto yeye ni jirani yake amemzoea”
Aidha Lutumo alieleza Jeshi la polisi linawashikilia watu 67 wanaotuhumiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya kiuhalifu ikiwa ni pamoja na wizi na kujihusisha na biashara haramu za madawa ya kulevya aina ya bangi na pombe ya moshi.
Kamanda huyo alieleza ,watu hao wanadaiwa kukutwa na mali kama pikipiki 10, silaha moja aina ya gobole, pombe ya moshi lita 13 na viroba vitatu vya bangi, puli 102 na kete 789 na dawa hizo haramu.
“Tumefanya msako kwa wiki mbili na tumefanikiwa na hii inatokana na ushirikiano kati yetu na wasamalia wema kwa kutupatia taarifa za siri,” alisema Lutumo.