Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisisitiza jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wakipokea taarifa ya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ludovick Nduhiye, akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wakipokea taarifa ya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), mkoani Morogoro.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) Eng. Mahmoud Chamle, akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wakikagua mitambo na vifaa vya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. John Ngowi (kulia), akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (katikati), mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) Eng. Mahmoud Chamle.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakisikiliza taarifa kutoka kwa Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) Eng. Mahmoud Chamle, wakati wakikagua mitambo na vifaa vya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), mkoani Morogoro.
PICHA NA WUU
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kuongeza nguvu kwenye Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), kwa kuitengea fedha za kutosha ili iweze kujiendeleza kwa kuwa na vifaa na mitambo ya kisasa, vitendea kazi, majengo na rasilimali watu kwa ajili ya kuwezesha kuzalisha mafundi wenye uwezo na ujuzi.
Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, mara baada ya kupokea taarifa ya Taasisi hiyo iliyoanzishwa kwa kuunganisha Chuo cha Taifa cha Ujenzi cha Morogoro na Chuo cha Teknolojia stahiki ya nguvu kazi cha Mbeya na kusisitiza uhitaji wa taasisi hiyo kuongezewa bajeti.
“Kamati inaomba Wizara muwe na dhamira ya dhati ya kukisaidia Chuo hiki ili kiweze kuimarika kwani kufanya hivyo mtazalisha waatalamu wa kutosha wenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo kwa kutumia teknolojia stahiki”, amesema Mhe. Kakoso.
Aidha, Kamati hiyo imesisitiza kuwa Taifa linategemea sana vyuo hivo kwani ndio msingi wa kupata mafundi wa ngazi ya kati na kuendeleza kusimamia na kuboresha miradi ya barabara na reli inayoendelea.
Kamati imeiagiza Wizara kuhakikisha Taasisi hiyo inapata wakufunzi wa kutosha wa fani zote ili kuongeza nguvu na ujuzi kwa wanafunzi watakaopata fursa ya kujiendeleza katika Taasisi hiyo na kusaidia Chuo kuongeza kutambulika Zaidi.
Awali akitoa taarifa kwa Kamati, Mkuu wa Taasisi hiyo Eng. Mahmoud Chamle, ameieleza kamati kuwa uanzishwaji wa taasisi hii utachangia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwani mafunzo yanayotolewa hapo yatawaandaa wahitimu kujiajiri zaidi.
Ameongeza kuwa Taasisi yake inatoa mafunzo ya muda mrefu katika fani za ujenzi, umeme, na mitambo katika ngazi ya Astashahda na Stashahada lakini pia inatoa mafunzo ya muda mfupi na mafunzo maalum kwa wahitimu wa fani za kihandisi na zinazoendana ili kuwaandaa na kuwajengea uwezo.
Ameendelea kusema kuwa kwa sasa Taasisi inaendesha mafunzo juu ya matumizi ya Teknolojia Stahiki ya Nguvu kazi katika kazi za ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara.
Kamati ya Miundombinu ipo mkoani Morogoro katika ziara yake ya kukagua miradi na kazi zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.