Afisa Uhusiano Mkuu wa EWURA, Bw Wilfred Mwakalosi akitoa elimu ya udhibiti wa shughuli za gesi ya kupikia kwa wadau waliotembelea banda la EWURA wakati wa Kongamano la Wadau wa gesi ya kupikia wa Afrika Mashariki leo Machi 15,2023 jijini Dar es Salaam.
Meneja Biashara ya Petroli EWURA, Bi Kemilembe Kafanabo akiwasilisha mada wakati wa kongamano la Wadau wa Gesi wa Afrika Mashariki ( EA LPG MEETING AND EXPO) leo Machi 15,2023 jijini Dar es Salaam
Afisa Mwandamizi Huduma kwa Wateja EWURA Kanda ya Mashariki, Bi Getrude Mbiling’i akitoa elimu ya namna Mamlaka inavyoshughulikia malalamiko ya wateja wakati wa kongamano la wadau wa gesi ya kupikia wa Afrika Mashariki leo Machi 15,2023 jijini Dar es Salaam
Sehemu ya washiriki wakifatilia mada mbalimbali wakati wa kongamano la wadau wa gesi ya kupikia ( LPG) linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia leo Machi 15 -16,2023
Na.Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), imeendelea kuwahamasisha Watanzania na wawekezaji wa ukanda wa Afrika Mashariki kuwekeza katika uhifadhi wa gesi ya kupikia (LPG) ili kukuza zaidi matumizi ya nishati hiyo nchini.
Meneja Biashara ya Petroli wa EWURA, Bi.Kemilembe Kafanabo, ametoa hamasa hiyo leo 15.3.23 wakati akiwasilisha mada kuhusu Usalama,Ubora,na Uhimili wa Gesi ya kupikia kwenye kongamano la wadau wa gesi ya kupikia ( LPG) linalofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 15-16 Machi 2023.
Bi Kafanabo ameeleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara hiyo, kwa kuondoa kodi kwenye bidhaa na mitungi ya kuwekea gesi ili kupunguza gharama za uwekezaji na kwa mtumiaji wa mwisho.
“Serikali imejizatiti kukuza matumizi ya gesi ya kupikia kwa kuondoa kodi kwenye bidhaa na mitungi, hivyo tuhamsike kuwekeza zaidi hususani kwenye miundombinu ya kuhifadhia” Alisisitiza Bi.Kemilembe.
Hata hivyo, uelewa mdogo miongoni mwa wadau kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia, uhimili wa gharama kwa watumiaji, miundombinu isiyokidhi viwango na ujazaji haramu wa mitungi ya gesi ya kupikia zimeendelea kuwa changamoto katika mnyonyoro wa biashara na matumizi ya gesi hiyo.
EWURA itaendelea kudhibiti ubora wa miundombinu na bidhaa, kuhakikisha usalama wake na matumizi sahihi ya bidhaa hiyo nchini.