Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
POLISI Konstebo Mwanaidi Shabani (25), askari wa Kituo cha Polisi Chalinze Mkoani Pwani,ambae alijeruhiwa katika ajali iliyotokea Machi 5 mwaka huu ,amefariki dunia .
Katika ajali hiyo, polisi wawili pamoja na karani wa mahakama walifariki dunia ,baada ya gari lenye namba za usajili T.323 BAL aina ya Toyota Crester likiendeshwa na mkaguzi wa polisi Ndwanga Dastan kuacha njia kisha kugonga karavati,na kusababisha vifo na majeruhi.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani Pius Lutumo, amesikitika kupokea taarifa ya kifo hicho na kutoa pole kwa Jeshi la polisi,ndugu na jamaa kwa kufikwa na msiba huo.
Alieleza,ajali hiyo ilitokea Machi 5 mwaka huu ,majira ya 11:45 huko maeneo ya Mavi ya Ng’ombe, Kijiji cha Mboga, Kata ya Msoga, Tarafa ya Chalinze, Wilaya ya Kipolisi Chalinze, barabara ya Chalinze/Segera Mkoa wa Pwani.
“Katika ajali hiyo mkaguzi msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani (28), askari wa kituo cha Polisi Chalinze, akitokea Chalinze kuelekea Lugoba, gari hiyo aliyokuwa akiiendesha liliacha njia kutoka upande wa kushoto wa barabara na kwenda upande wa kulia na kugonga karavati kisha gari hilo kupinduka na kusababisha vifo vya watu wa tatu pamoja na majeruhi mmoja na uharibifu wa gari hilo”
Waliofariki kwenye ajali hiyo alikuwa ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Ndwanga Dastani miaka 28 – aliyekuwa dereva wa gari,Polisi Konstebo Emmiliana Charlse miaka 26 – askari wa kituo cha Polisi Chalinze, na Karimu Simba miaka 27 – karani wa mahakama ya Wilaya ya Lugoba.
“Marehemu Konstebo Mwanaidi Shabani , askari wa Kituo cha Polisi Chalinze yeye aliumia maeneo mbalimbali ya mwili wake na alipelekwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.””ambapo amefariki Machi 14 ,na Machi 16 anatarajia kuzikwa “
Lutumo alisema ,chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni mwendokasi na dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka.