Na. Asila Twaha, TAMISEMI
Serikali imewataka wauguzi na wakunga kusimamia maadili na miiko ya kazi zao kwa kutoa huduma bora kwa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wauguzi na wakunga katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameeleza kuwa ili mgonjwa aridhike na huduma inayotolewa kwenye vituo vya afya ni vyema kushirikiana kuanzia ngazi ya chini mpaka juu lengo likiwa ni kutoa huduma bora kwa jamii.
Amewataka kuendana na mahitaji ya watu wanaowahudumia kwa kuwa wanapokuja kupata huduma za kiafya wanaimani kupata huduma bora.
“mbali ya kujiiona ni waajiriwa unalipwa mshahara lakini pia tuna fungu letu kwa mungu kazi ya uuguzi na ukunga ni ibada niwashuauri tutekeleze majukumu yetu kwa upendo na imani” amesema Dkt. Shekalaghe
Amewataka kuzingatia miiko na kufuata maadili ya kazi zao kwa kuwa itasaidia wagonjwa kuwa na imani na huduma inayotolewa lakini watakua na imani na watoa huduma.
Ameeleza Serikali inatambua na kuthamini kazi wanazozifanya na pia inajua uwepo wa baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo Serikali itaendelea kufanyia kazi .
Ametoa rai kwa watendaji hao kuendelea kufanya kazi ikiwa wao ndio wanaempokea mgonjwa kwa hatua ya awali mpaka kujua maendeleo yake.
Amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kutoa huduma iliyokuwa bora kwa wananchi.
“pendaneni, shirikianeni ninyi mkishirikiana mtaweza kutoa huduma iliyobora sababu itakuwa mnafanya kazi kama wamoja”
Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bi. Amina Mfaki akimuakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe amewataka watendaji hao kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya nchini.
Aidha, ametoa rai kwa viongozi wanatoka katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia maadili ya kazi ili kuepusha vitendo vinavyoweza kuharibu kazi na taswira ya kada hiyo.