Wahitimu wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Mwenge wakiwa kwenye mahafali ya 48 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mkoani Singida.
…………………………………………………
.Na Dotto Mwaibale, Singida
WAHITIMU wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida mkoani hapa wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa yakutojiingiza kwenye vishawishi
vya kupata ufadhili wa masomo nje ya nchi na kujikuta wakiingia kwenye mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja kupitia mitandao.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Mussa Sima, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 48 ya kidato cha sita katika
shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Sasa hivi zinatumika mbinu
mbalimbali na mataifa ya magharibi kama mnavyoona jinsi serikali yetu
inavyopambana na masuala ya ushoga na usagaji
wanaweza kutengeneza mbinu ya wewe kuingia katika shughuli hizo za
maadili ambayo sisi hatuna hivyo mnapaswa kuwa makini sana mnaweza kuhitaji
kupata maisha ya haraka na mkajikuta
mmeingia kwenye vitendo hivyo,” alisema Sima.
Alisema Serikali haikubaliani na mambo hayo lakini mitandao ya kijamii
imetoa nafasi ya mtu kufanya chochote lakini Serikali yetu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezuia vitu ambavyo havina maadili na utamaduni wa kitanzania mfano masuala ya ushoga na picha za utupu.
Sima alisema kutokana na kukua kwa teknolojia mtu anaweza akaingia kwenye
mitandao ya kijamii na kukutana na viti hivyo vikiwepo kupata hela au ufadhili wa masomo
na bila kujua anajiingiza kujaza fomu kupatiwa ufadhili wa masomo au
kazi na kutumiwa fedha na tiketi ya ndege.
Mbunge Sima alisema watu hao wakija na mbinu hizo za kutoa ufadhili wa
masomo katika vyuo mbalimbali nje ya nchi walengwa wanatakiwa kutoa taarifa kwa
wizara husika ambayo inavijua vyuo vyote hivyo ili kupata uthibitisho badala ya
kwenda kimya kimya na kujikuta wakiharibikiwa.
Aidha, Sima aliwataka wazazi na walezi wa wahitimu hao watakapokuwa nyumbani wakisubiri matokeo yao kuwapa stadi
za maisha kwa kuwafundisha shughuli
mbalimbali za nyumbani ikiwemo ujasiriamali, kilimo ama kujihudumia hatua
itakayowasaidia kujitambua na kujilinda katika kipindi hicho.
Pia Mbunge Sima alitoa Sh.Milioni 1
kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa chumba maalumu cha kuhifadhi
nyaraka mbalimbali na mitihani baada ya Mkuu wa Shule hiyo, Method Njiku
kuelezea changamoto ya kutokuwa na chumba hicho.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo Njiku alisema kuwa imeendelea kufanya vizuri
na kushika nafasi ya juu katika matokeo ya mitihani ya taifa na kuwa mikakati
waliyonayo ni kuondoa kabisa daraja la nne na kubakiwa na daraja la kwanza na la
pili.
Njiku alisema siri ya mafanikio hayo inatokana na kujiweka
malengo, mikakati na kuhakikisha inatekelezwa kwa wakati na kuwa miongoni mwa
mikakati hiyo ni kufundisha masomo ya ziada na rekebishi, kutoa motisha kwa
walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo, ushirikiano baina ya bodi
ya shule, wazazi, wafanyakazi wanafunzi na wadau wengine wa elimu.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Kilanja Mkuu Mstaafu wa Shule hiyo, Makindoya
Shaban alielezea changamoto kadhaa kuwa ni pamoja na ukosefu wa uzio jambo
ambalo huathiri usalama na wakati mwingine kuchochea utovu wa nidhamu kwa
wanafunzi na utoro.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa vifaa vya kufundishia
somo la kompyuta na kuwafanya kushindwa kupata maarifa, ujuzi na umahiri wa
elimu ya kidigitali sambamba na kutokuwa na gari ambalo litawasaidia katika
ziara za masomo.
Shaban alisema Shule ya Sekondari Mwenge ni moja ya shule kongwe hapa
nchini na kuwa waanzilishi wa shule hiyo ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) ambao waliikabidhi kwa Serikali mwaka 1967 kama zawadi ya
kuunga mkono malengo ya Azimio la Arusha.
Taswira ya mahafali hayo.
Afisa Elimu Kata ya Majengo, Mwalimu Nuru Ntandu akizungumza kwenye mahafali hayo.
Burudani ikitolewa.
Burudani zikiendelewa kutolewa.