Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera aliyevaa miwani akionyeshwa namna mashine ya kisasa ya kupimia uwiano wa matairi ya gari (Wheel Balance) inavyofanya kazi wakati akikagua vitendea kazi vilivyopo katika karakana ya TEMESA mara baada ya kufungua rasmi kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana hiyo Tarehe 10 Machi 2023. Kikao hicho kimefanyika katika eneo la karakana hiyo iliyopo Sabasaba Mbalizi Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera katikati akikagua vifaa vinavyotumika kufanyia matengenezo kinga (Service) ya magari katika karakana ya TEMESA Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya kufungua rasmi kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda na kushoto ni Meneja wa TEMESA Mbeya Mhandisi Said Mawazo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akiwa katika picha ya pamoja na mafundi wa karakana ya TEMESA Mbeya mara baada ya kufungua rasmi kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana hiyo Tarehe 10 Machi 2023. Kikao hicho kimefanyika katika eneo la karakana hiyo iliyopo Sabasaba Mbalizi Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akikabidhiwa cheti cha shukrani na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda kwa mchango ambao ofisi ya Mkoa wa Mbeya inatoa kwa TEMESA ikiwemo kulipa madeni ya huduma wanazopatiwa kwa wakati wakati. Zoezi hilo limefanyika Tarehe 10 Machi 2023 wakati wa kikao cha wadau wanaotumia huduma za TEMESA kilichofanyika katika eneo la karakana hiyo iliyopo Sabasaba Mbalizi mjini Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera (aliyevaa miwani na Kaunda suti mbele) akionyeshwa vifaa vinavyotumika kufanyia matengenezo ya magari katika karakana ya TEMESA Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya kufungua rasmi kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana hiyo. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA Mhandisi Hassan Karonda na Meneja wa TEMESA Mbeya Mhandisi Said Mawazo. Anayempatia maelezo ni Mhandisi Zephrine Bahyona.
Meneja wa Kikosi cha Umeme TEMESA Mhandisi Pongeza Semakuwa aitoa mada wakati wa kikao cha wadau wanaotumia huduma za TEMESA Mbeya kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la karakana hiyo iliyopo Mtaa wa Sabasaba Mbalizi mjini Mbeya. Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kikiwa na lengo la kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na karakana hiyo.
PICHA ZOTE NA SAMSON MRUTU (TEMESA)
***********************
Na. Alfred Mgweno (TEMESA Mbeya)
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amezitaka Taasisi za Serikali zilizoko Mkoani Mbeya kuanza kutengeneza magari ya Taasisi zao na mitambo katika karakana za Wakala huo kwakua Wakala huo kwa sasa umejizatiti na uko tayari kusimamia huduma hizo kwa weledi na ufanisi mkubwa. Mhe. Homera ameyasema hayo Tarehe 10 Machi, 2023 wakati wa kikao cha wadau wanaotumia huduma za karakana ya TEMESA Mbeya kilichofanyika Karakana ya Wakala huo iliyoko eneo la Sabasaba kata ya Mbalizi mjini Mbeya.
Akizungumza katika kikao hicho cha wadau, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ametoa wito kwa Taasisi zote za Umma kuendelea kutumia huduma za Wakala huo kwani kwa sasa TEMESA iko vizuri na imejipanga vizuri. ‘’Kulikua na fikra huko nyuma, ukiangalia TEMESA ukipeleke gari unasema kwamba hali ni mbaya, lakini sasa TEMESA ya Awamu ya Sita ni TEMESA ya vitendo, hongera sana TEMESA kwa mabadiliko haya nimeshuhudia kwa macho yangu vifaa vya kisasa vimefungwa hapa, sasa naagiza Taasisi zote za Umma njoeni mtengeneze magari yenu hapa, watakadiria na watatengeneza kwa weledi wa hali ya juu sana, vinginevyo tutaendelea kupata hasara kwa kupeleka magari yetu mitaani ambako wanatengeneza magari ndani ya siku mbili tatu yanaharibika, hapa wana mitambo mizuri, na wana vitendea kazi na vifaa vizuri na vya kisasa ambavyo wamewezeshwa na Serikali’’ Amesema Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Homera pia amewashukuru wadau hao kwa kujitokeza kwenye kikao hicho ili kutoa mrejesho wa huduma wanazopatiwa na kusema kuwa uwepo wake katika kikao hicho si wa bahati mbaya bali amefika hapo kwa ajili ya kuangalia ufanisi wa TEMESA kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
‘’Hii inatuonyesha kwamba TEMESA ile ya Awamu zingine sio sawa na ya Awamu ya Sita, ni TEMESA tofauti kidogo ndio maana tumekuja kuangalia vifaa walivyonavyo na tumeshuhudia kwamba mabadiliko ni makubwa, kwahiyo kipekee kabisa tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuibadilisha TEMESA na kuwa TEMESA ambayo imebadilika sana kwa usimamizi mkubwa wa ndugu yetu Lazaro Kilahala, mimi niseme tu kwamba Mhe. Rais ameweka zaidi ya shilingi milioni 700 kwenye ununuzi wa vifaa nchi nzima, haya ni mafanikio makubwa sana na tumpongeze sana Mhe. Rais.’’ Alisisitiza Mhe. Homera
‘’Lakini pia nisisitize, wadau tulipe madeni, kama tulivyoambiwa kwenye hotuba, TEMESA anadai Taasisi za Umma Zaidi ya shilingi Bilioni 3.8, na wakati huo huo wanadaiwa na wazabuni Bilioni 3.7, hiki ni kiasi kikubwa sana kwa Taasisi ya Umma kudaiwa, hivyo niombe wale wote wanaodaiwa andika barua uki waorodhesha na majina ya Taasisi zao, leta tuanze kuwaandikia barua ili walipe hayo madeni ili TEMESA iweze kuwahudumia vizuri Watanzania.’’ Alimaliza Mhe. Homera.
Mhe. Homera alitoa pongezi pia kwa Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Said Mawazo kwa kutekeleza maagizo yake ambayo aliyatoa mwaka jana akiagiza ifikapo Tarehe 15 mwezi Novemba mwaka 2022, zifungwe taa za kisasa eneo la Ijinda na agizo hilo lilitekelezwa.
‘’Hongera sana Mhandisi Mawazo, huo ndio utendaji tunaoutaka, utendaji wa mfano, utendaji ambao unajali muda wa Watanzania, na Watanzania hawa wanahitaji huduma hawahitaji maneno’’, Alisema Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa pia aliwataka TEMESA kuwa na watumishi waadilifu, kuboresha huduma kwa kuweka gharama za uhalisia, kujenga mazingira ya uaminifu kwa wadau wake ili kurejesha Imani ambayo wadau hao walikua wameipoteza kwa muda mrefu na pia kuhakikisha wanatengeneza mazingira ya kuwavutia wadau hao kurudi kutumia huduma za Wakala huo.