CHAMA Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) leo Machi 11,2023 kimeandaa Kongamano la wazi la kukusanya maoni ya wadau juu ya namna ya kuboresha taasisi za Haki Jinai nchini.
Akizungumza katika Kongamano hilo ,Meneja Programu wa TLS , Mackphasan Mshana amesema miongoni mwa mapendekezo waliyoainisha ni pamoja na kuundwa kwa chombo huru kitakachosimamia Taasisi za Haki Jinai,makosa yote yapatiwe dhamana ili kupunguza msongamano kwenye mahabusu na watu wasikamatwe kabla ushahidi haujakamilika.
“Tunapendekeza ili hizi taasisi zisijifanye wanavyotaka kuwe na chombo huru kinachowafatilia namna wanavyofanya kazi na endapo kuna ukiukwaji wa haki waadhibiwe ,”alisisitiza.
Mshana amesema TLS ni wadau muhimu kwani jukumu lao ni kusaidia serikali na taasisi zake kuangalia mifumo yote ya kisheria na mifumo inayosimamia sheria kwamba inaendana na matakwa ambayo wanayo na inaendana na utawala wa kisheria.
Pamoja na hayo amesema kuwa maoni yatakayotolewa na kukusanywa yatasaidia tume kuandaa mapendekezo ambayo yatapelekwa ngazi ya serikali kwaajili ya maboresho.
“Tumefanya kongamano la wazi kwasababu kumekuwa na malalamiko kwa taasisi ambazo zinahusika katika mfumo wa haki jinai jinsi unavyofanya kazi hasa taasisi zinazosimamia sheria kama mahakama,polisi,magereza,TAKUKURU, dawa za kulevya,”alieleza.