Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Comrade Juma Zuberi Homera amewataka makamanda wa Polisi wa mikoa ya nyanda za juu kusini, Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe kushirikiana katika kuzuia na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji binadamu katika mikoa yao.
Mhe.Homera ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku moja cha Makamanda wa Polisi wa mikoa mitano ya nyanda za juu kusini, Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe kilichohusisha pia wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, wakuu wa operesheni na wakuu wa usalama barabarani, Machi 11, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mbeya.
Mhe.Homera amewataka makamanda kuwakamata waganga wapiga ramli chonganishi, kupeleleza kesi zao na kisha kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria kwani wamekuwa wakisababisha mauaji yatokanayo na imani potofu za kishirikina.
Aidha Mhe.Homera amesema kuwa, ili kukabiliana na uingizaji na usambaa wa noti bandia katika mzunguko wa fedha, amezungumza na Gavana wa Benki Kuu kuanza utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi na Jeshi la Polisi ili kuwajengea uwezo katika kubaini noti bandia.
Sambamba na hilo, Mhe.Homera amewataka wakuu wa kikosi cha usalama barabarani (RTO) kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani kutokana na mwendo kasi na ku over take katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe ACP Hamis Issah kwa niaba ya makamanda wengine, ameeleza kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kupanga na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia, kudhibiti na kupambana na uhalifu na ajali za barabarani kwa mikoa mitano ya nyanda za juu kusini. Aidha ameongeza kuwa kikao hicho ni chachu katika kuongeza ushirikiano miongoni mwao hasa katika kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu.
Imetolewa na,
BENJAMIN E. KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.