Meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma ,Dk Maguha Stephano kutoka Taasisi ya saratani Ocean road akizungumza na madaktari na wauguzi katika hospitali ya ALMC Selian kuhusu maswala ya saratani.
Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha wakipata elimu juu ya maswala ya saratani walipofika kupata huduma hiyo katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru.
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha .Wananchi mbalimbali mkoani Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani unaotolewa bure na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya saratani Ocean Road kwa kushirikiana na Hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru.
Aidha huduma hiyo ya matibabu ambayo ilianza machi 6 na itamalizika machi 10 tayari , Jumla ya wanawake 351 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti .
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Meneja kitengo cha uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road ,Dk Maguha Stephano wakati akizungumza katika kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya saratani inayoendelea katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mount Meru ambayo imefadhiliwa na Benki ya NBC.
Amesema ,kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wagonjwa wa saratani mwaka hadi mwaka ambapo wagonjwa wengi hufika hospitali katika hatua za mwisho kabisa ambapo taasisi hiyo imeona kuna umuhimu wa kuandaa mpango huo na kwenda katika hospitali hiyo kwa ajili kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa awali wa saratani.
Dk.Maguha amesema wanawake 351 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango na matiti na kati yao wanawake 7 wamekutwa na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi na kufanyiwa matibabu huku wanawake 4 wakikutwa na viashiria vya saratani ya mlango wa kizazi na wengine 9 wakikutwa na vivimbe katika matiti yao na hivyo kufanyiwa vipimo zaidi na madaktari bingwa wa Patholojia kwa uchunguzi zaidi.
“Kupitia kambi hii pia tumeweza kupima saratani ya tezi dume ambapo jumla ya wanaume 100 wamefanyiwa vipimo na kati ya hao wanaume 7 wamekutwa na viashiria vya saratani ya Tezi dume na hivyo wanatakiwa kufanyiwa vipimo zaidi
“amesema Dk. Maguha.
Aidha amesema kuwa,lengo la kambi hiyo ni kutoa elimu ya magonjwa ya saratani kwa wananchi wa Arusha na kutoa huduma ya uchunguzi wa awali wa saratani bila malipo na kuwezesha ugunduzi wa mapema wa saratani katika hatua za awali kwa wananchi wa Arusha.
“Lakini pia kupitia kambi hii ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Ocean Road tumeweza kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi kati ya madaktari wetu na madaktari wa hospitali ya rufaa Mount Meru na hospitali ya ALMC Selian kuhusu magonjwa ya saratani .”
Ameongeza kuwa, kanzi data ya Taasisi hiyo kwa mwaka 2021 zinaonyesha kwamba wagonjwa kwa upande wa Wanawake aina za saratani zinazoongoza ni pamoja na saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 47,ikifuatiwa na saratani ya matiti kwa asilimia 18 na saratani ya koo kwa asilimia 4 huku kwa upande wa wanaume saratani ya koo la chakula likiongoza kwa asilimia 18 ikifuatiwa na saratani ya tezi dume kwa asilimia 11
Hata hivyo amesema ,njia mbalimbali za kujiepusha na saratani ni pamoja na kupunguza matumizi ya mafuta mengi katika vyakula hasa yale ya wanyama na kupunguza unene uliokithiri na kula matunda na mboga mboga kwa wingi ,kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kupitia kiasi ,huku akiwakumbusha wananchi wa Arusha kufanya uchunguzi mara kwa mara hata kama hawana dalili zozote za ugonjwa.
Baadhi ya wagonjwa waliofika kupata huduma katika kambi hiyo, Janeth Laizer na Dismas Mollel wamesema kuwa, wanashukuru kwa jinsi ambavyo taasisi hiyo imeweza kujitolea na kuja kufanya matibabu ya saratani kwani yanawasaidia sana kuweza kupata matibabu ya awali na kuweza kupata matibabu mapema.