Adeladius Makwega-WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Machi 10, 2023 amesema kuwa Tanzania imeteuliwa kuwa Mjumbe katika Bodi ya Ushauri Jumuiya ya Madola kwenye Michezo (CABOS) na hatua hiyo inatokana na kuimarika kwa nyanja za diplomasia ikiwemo michezo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Taarifa iliyotolewa na Waziri Chana na kulifikia dawati la Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizarani hapo imesema,
“Kwa uteuzi huo, Bw. Alli Mayay (Tembele) sasa anaiwakilisha Tanzania katika Bodi ya CABOS na kuwa Mjumbe mwakilishi wa Bara la Afrika huku Bw. Mayay kwa sasa ndiye Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Michezo nchini.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa CABOS ni chombo cha kumshauri Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Serikali wanachama kuhakikisha kunakuwepo ushirikishwaji thabiti wa Serikali na uwakilishi katika maendeleo ya sera na utekelezaji wake kwa kuzingatia maadili na matarajio yaliyowekwa ndani ya Mkataba wa Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ndugu Saidi Yakubu amesema kuwa kwa uwakilishi huo, Tanzania imekidhi vigezo vya uanachama wa CABOS na itafanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na thabiti na wanachama wengine wapya na wanaorejea kutoka kila eneo la Jumuiya ya Madola kutoka Afrika, Asia,Karibiani, Amerika, Ulaya, pamoja na Pasifiki.
Tanzania inakuwa mjumbe CABOS kwa miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2023-2015
Michezo ya Jumuiya ya Madola inayohimiza michezo kwa maendeleo ya amani ulimwenguni ilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Canada mwaka 1930, hadi sana inajumuisha mataifa kadhaa yaliyokuwa chini ya Utawala wa Uingereza hata hivyo nchi nne za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Madola ni Rwanda, Msumbiji, Gabon, na Togo-hazina uhusiano wa kihistoria na Dola ya Uingereza.