Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Simanjiro Mkoani Manyara, Anna Shinini ameongoza harambe ya kuchangia ujenzi wa darasa la shule ya awali la Kanisa la KKKT na kupatikana shilingi 1,840,000.
Anna Shinini ameongoza harambee hiyo akiwa mgeni rasmi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambapo alikuwa mgeni rasmi wa wanawake wa KKKT, mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro.
Akizungumza baada ya harambee hiyo Shinini amewapongeza wanawake hao walioshiriki maadhimisho hayo na kujitolea kuchangia ujenzi wa darasa hilo la awali.
“Tunamshukuru Mungu tumeendesha harambe ndogo na kufanikisha kupatikana kwa kiasi hiki cha fedha shilingi 1,840,000 kwenye maadhimisho hayo ya wanawake dunia,” amesema Shinini.
Hata hivyo, amewapongeza wanawake hao wa KKKT kwa kumwalika yeye kushiriki nao maadhimisho akiwa mgeni rasmi kupitia nafasi yake ya Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya ya Simanjiro.
“Nashukuru kwa kutambua uwepo wangu kupitia UWT na kunialika kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho haya pamoja na kuwa ni Mwenyekiti wa UWT,” amesema Shinini.
Amesema wanawake hao wanapaswa kupinga ukatili wa kijinsia kwani ni uovu na kufunge kwa maombi kwani watoto wanaharibikiwa hivyo tunzeni familia, watoto na baba.
Amewataka wanawake hao watunze mazingira na kuhifadhi mazingira kwani ni uumbaji wa Mungu, wanawake ni jeshi kubwa hivyo wazingatie hilo.
Hata hivyo, amewataka wanawake hao wajitahidi kuwalea watoto wao vyema kwani ni jukumu lao kufanya kazi kwa jamii japokuwa majukumu ya mama ni kulea familia.
“Mtimize majukumu yenu ipasavyo ila msiwadanganye watoto katika malezi na makuzi, tuwe wa kweli, mwambie ukweli mtoto kuwa nasafiriki, badala ya kusema naenda kuchota maji kumbe umesafiri,” amesema Shinini.
Amewapongeza wanawake hao ambao ni jeshi kubwa kwa kupendeza na mavazi waliyoyazaa siku hiyo pia wapendeze kwenye mioyo yao kwa kila wakati.
“Nawapongeza kwa usafi mnavyoonekana leo kwani mlivyopendeza muwe mnapendeza kila siku na pia usafi wa mwili uendane na usafi wa roho,” amesema Shinini.
Amewataka kutambua umuhimu wa wanawake kwa jamii kwani hata kwenye biblia imezungumzwa kuwa mwanamke akiomba Mungu anasikia maombi yao mara moja hivyo wawaombee viongozi.
Amewasihi wanawake hao kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, kila wakati ili aweze kutimiza vyema majukumu yake na pia wamzungumzie kwa mema wasimnenee mabaya.