Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil abdallah (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali (kushoto)katika kikao kifupi cha kujadili miradi ya Kimkakati.
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil abdallah pamoja na wataalam wa wizara hizo katika kikao kilichofanyika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma wakijadili kuhusu mkakati wa kuendeleza madini mkakati.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali katika kikao hicho.
Dodoma
Wizara ya Madini na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zimeazimia kuanza utekelezaji wa miradi ya Kimkakati katika Sekta Madini ikihusisha miradi ya Liganga na Mchuchuma ili iweze kuanza kwa wakati.
Hayo yameelezwa wakati wa kikao cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil abdallah kilicholenga kujadili miradi hiyo ya Kimkakati.
Miradi mingine iliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na mradi wa chuma ghafi na makaa wa Maganga Matitu na Mgodi wa Katewaka pamoja na mradi wa Magadi Soda katika bonde la Engaruka.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Mahimbali amesema, miradi hiyo itatekelezwa mapema na kwa wakati ili rasilimali hizo zilinufaishe taifa na watanzania.
Aidha, Mahimbali ameahidi kuwa wizara yake itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara muda wote inapohitajika ili shughuli za utekelezaji wa miradi hiyo uweze kuanza kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Dkt. Abdallah amemshukuru Katibu Mkuu Mahimbali kwa kufungua mazungumzo ya utekelezaji wa mchakato huo wa kutekeleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa ushirikiano na wizara yake.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abdallah amempongeza Katibu Mkuu Mahimbali kwa kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Amesema Wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha ili wizara hizo zilete tija kwa watanzania hususan katika utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Wizara ya Madini mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na kimehudhuriwa na wataalam mbalimbali wa wizara hizo mbili.