Mratibu wa ziara ya waandishi wa habari katika eneo linalosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB), Constantine Akitanda akipanda mti rafiki na maji kwenye eneo Mwakangaga kata ya Ubaruku wilayani Mbarali Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Kanali Denis Mwila akizungumza na waandishi wa habari waliopo katika ziara ya kutembelea Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB) Mhandisi Abisai Chilunda wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB), wilayani Mbarali mkoani Mbeya, akiwaeleza waandishi wa habari namna wanavyoshiriki kudhibiti uharibifu mazingira katika eneo hiloKatibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji Mto Mbarali Chini (JUAMBACHI), Idrisa Nyahove akitoa maelezo kwa Ofisa Maendeleo ya Jamii RBWB, Pendo Rugalla na Mratibu wa ziara ya waandishi katika bodi hiyo Constantine Akit Muonekano wa Mto Mbarali Chini katika kijiji cha Mwakaganga kata ya Ubaruku, likionekana limeharibika kwa shughuli za kilimo
Muonekano wa Mto Mbarali Chini wilayani Mbarali mkoani Mbeya ukitiririsha maji.
*******************************
Na Selemani Msuya, Mbarali
MSUKUMO wa kisiasa na kipato vimetajwa kuwa sababu kubwa inayochangia ongezeko la uharibufu wa vyanzo vya maji na mazingira kwenye Mto Mbarali Chini wilayani Mbarali mkoani Mbeya, unaosimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (WBWB).
Hayo yameainishwa na Katibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji Mto Mbarali Chini (JUAMBACHI), Idrisa Nyahove wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo na kujionea hali ya wananchi hasa wakulima kulima katika eneo la mto ambalo ni mita 60.
Nyahove amesema JUAMBACHI wilayani Mbarali inahusika kusimamia vijiji sita vya Mwakaganga, Ibohora, Mayota, Itamba, Msusuli na Warumba ambavyo wananchi wake wananufaika na maji ya Mto Mbarali Chini kwa shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na matumizi ya nyumbani.
Katibu huyo amesema wao kama wana jumuiya wamekuwa wakipambana kuzuia wananchi kufanya shughuli za uzalishaji kwenye vyanzo vya maji, ila kuna nguvu ya wanasiasa katika kukwamisha lengo hilo, hivyo ameomba Serikali kuongeza nguvu ili waweze kufanikiwa.
“Tumekuwa tukiwakamata na kuwazuia watu ambao wanaharibu vyanzo vya maji, ila sisi kama JUAMBACHI tunakutana na changamoto hasa ya wanasiasa wa kata ya Ubaruku, hivyo naomba viongozi wa serikali katika ngazi zote waingie katika kusaidia utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji,” amesema.
Amesema wanasiasa wengi katika ukanda huo wa Mto Mbarali Chini wanafikiria kupata kura na sio uendelezaji wa rasilima maji ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi.
Nyahove amesema pamoja na wanasiasa kukwamisha shughuli za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji, bado kuna msukumo wa wananchi kutaka kupata kipato kwa ajili ya maisha yao ya kila siku, hali ambayo inawatoa ufahamu kuhusu uhifadhi na utunzaji mazingira.
Katibu huyo amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo ya uharibifu wamekuwa wakikutana na vitisho kutoka kwa wakulima na wanasiasa, lakini kwa kushirikiana na uongozi wa bonde hawatarajii kurudi nyuma.
Amesema katika kupambana na hali hiyo wamekuwa wakipanda miti na kushiriki kuweka alama za mipaka (Bikoni), lakini bado kuna watu wanakiuka na wao wanawachukulia hatua za kisheria.
“Tunakutana na vitisho vingi, lakini kwa sababu tunatambua kila nafsi itaonja umauti hatutarajii kurudi nyuma, kwani tunaamini maji ni uhai, hivyo hatupo tayari kurudi nyuma. Tunasisitiza Serikali iongeze nguvu ili RBWB iweze kufanikisha lengo la utunzaji na uhifadhi vyanzo vya maji,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mazingira JUAMBACHI, Agnes Lupenza amesema wakulima na wafugaji wamekuwa kikwazo kikubwa katika shughuli zao za kila siku.
Amesema jamii ya wafugaji imekuwa ikiwatisha wanapoenda kuwaondoa katika maeneo ambayo hawaruhusiwi kuwepo.
Lupenza amesema, ili kufanikisha zoezi la utunzaji na uhifadhi wa rasilimali maji na mazingira ni jukumu la kila mdau kushiriki kivitendo.
“Wapo wanasiasa ambao wanafatua matofali, wamekuwa kikwazo kikubwa sana katika kusimamia uhifadhi na utunzaji mazingira, lazima tushirikiane kuwaondoa,” amesema.
Mhandisi Abisai Chilunda wa RBWB Mbarali, amesema wamekuwa wakishirikiana na jumuiya na serikali kuhakikisha rasilimali maji inatumika kwa mujibu wa sheria, ila bado zipo changamoto.
Chilumba amesema katika kufanikisha hilo wameweza kuweka alama za mipaka na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote ambao wanakiuka sheria za maji.
“Maji ni kama dhahabu, hivyo hatuwezi kumvumilia mtu yoyote anayeshiriki kuharibu vyanzo vya maji, hadi sasa tumevunja mabanio matano makubwa ambayo ni Banio la Nguvu Kazi Mwanazala, Kapunga, Igurusi, Mjabaja na mengine, ila zoezi hilo la ubomoaji ni endelevu,” amesema,
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila, amesema Serikali haitamvumilia mwananchi yoyote ambaye atabainika kuharibu vyanzo vya maji katika eneo lake la uongozi.
Kanali Mwila amesema maji yanayotoka katika wilaya hiyo yana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hasa katika uzalishaji wa nishati ya umeme na kilimo.
“Maji yanayopita Mbarali yanazalisha umeme Mtera, Kihansi, Kidatu na siku chache zijazo tunatarajia kupata megawati 2,115 katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), hivyo tutashirikiana na watu wa bonde kuhakikisha vyanzo hivi vinakuwa endelevu,” amesema.
Mwisho.