Na Victor Masangu,Kibaha
Baadhi ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya mji Kibaha bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ukosefu wa mahitaji muhimu ikiwemo taulo za kike.
Kwa kuliona hilo wafanyakazi wanawake wa kampuni ya SF Group ya Jijini Dar es Salaam wameamua kutumia maadhimisho siku ya wanawake duniani kufanya matendo ya huruma katika kata ya sofu kwa baadhi ya maeneo.
Wafanyakazi hao wa SF group ambao wameona kuna haja ya kuitumia siku hiyo hivyo kuungana kwa pamoja na kwenza kutoa misaada mbali mbali kwa wanafunzi wa shule ya Koka sekondari pamoja na kituo Cha watoto yatima na wanaishi katika mazingira magumu.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake katika ziara hiyo Aisha Kanyika alisema kwamba wametoa msaada wa vitu mbali mbali katika shule ya Koka sekondari ikiwemo taulo kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili ziweze kuwasaidia kusoma katika mazingira rafiki.
“Mimi pamoja na wenzangu tupo hapa kwa ajili ya kutoa msaada wa vitu mbali mbali katika shule hii ya Koka sekondari na pia tunamshukuru Mwenyekiti wetu wa SF mheshimiwa Koka pamoja na mkewe ambao wameweza kuhakikisha wanafanikisha shughuli hii,”Alibainisha Aisha.
Aidha Aisha alisema kwamba lengo lao ni kuendelea kuisaidia jamii katika nyanja mbali mbali na kuwahasa wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo ambayo wamejiwekea katika siku za baadae na kuwa ni nidhamu kwa walimu wao.
Pia katika ziara hiyo wafanyakazi hao walitembelea kituo Cha watoto yatima na ambao wanaishi katika mazingira magumu ambapo walitoa msaada wa vyakula mbali mbali ikiwemo unga,mafuta ya kupikia,madaftari,maji ya kunywa,miswaki na mahitaji mengine muhimu pamoja na fedha.
Naye Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya Koka Sekondari Godwin Magoha aliwashukuru wafanyakazi hao kwa moyo wa kujitolea na kwenda kutoa msaada wa vitu mbali mbali ambavyo vitakuwa ni msaada hasa kwa watoto wa kike.
Kwa upande wake Mkurugenzi ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha Buloma Anna Kiando amebainisha kwamba amefurahishwa sana na kitendo cha wafanyakazi hao wa SF Group kutenga muda wao na kutoa msaada kwa watoto hao ambao kwao ni mkombozi mkubwa kulingana na mahitaji waliyopatiwa.
Elina Mgonja ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji naye hakusita kuwapongeza wafanyakazi hao kwa kuonyesha uzalendo kwa watu wenye mahitaji pamoja na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji Silvestry Koka pamoja na mke wake kwa kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji.
Ziara ya wafanyakazi wanawake wa kampuni ya SF Group katika kata ya sofu imeleta neema kubwa kwa wanafunzi wa kike katika shule ya Koka sekondari pamoja na kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Buloma kutoka na misaada waliyopatiwa.