Baadhi ya wanawake wa mkoa wa Ruvuma wakicheza muziki wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo katika mkoa wa Ruvuma imefanyika katika viwanja vya Bandari wilayani Nyasa.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thoma,s akikabidhi kitabu cha mwongozo wa baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi wa mkoa huo kwa mwenyekiti wa jukwaa hilo Joun Ngapomba,kulia Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya.
Mfanyakazi wa kiwanda cha kukoboa kahawa cha MCCCO Mbinga Nikolatha Hyera kushoto,akimpa zawadi ya kahawa inayokobolewa na kiwanda hicho Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas aliyetembea banda la kiwanda hicho wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya Bandari wilayani Nyasa.
Mkurugenzi wa kampuni ya Super Feo &Selou Express Omari Msigwa akiwasalimia wananchi na viongozi wa serikali ya mkoa wa Ruvuma waliodhuria maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake Duniani ambayo katika mkoa wa Ruvuma yamefanyika wilayani Nyasa.
Na Muhidin Amri,
Nyasa
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amekemea tabia ya baadhi ya wanawake hapa nchini, kuwa chanzo cha kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ushoga tabia inayozidi kuongezeka katika jamii.
Kanal Laban ametoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na wananchi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya Bandari katika mji mdogo wa Mbambabay wilayani Nyasa.
Amewataka wanawake katika mkoa huo kushirikiana na kusaidia katika shughuli mbalimbali ili kujiletea maendeleo yao.
Kanal Laban, amewaonya kuacha tabia ya kuchukiana miongoni mwao kwa kuwa inawarudisha nyuma na kuwapunguzia nguvu pale wanapodai haki zao za msingi katika vyombo vya maamuzi,sehemu za kazi na katika jamii inayowazunguka.
Aidha Mkuu wa mkoa alisema,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imesimama kidete kwa kutetea na kutoa haki kwa wanawake hapa nchini na kuwapa fursa na nafasi mbalimbali za uongozi na kwenye vyombo vya maamuzi.
Amewaomba wananchi hususani wanawake katika mkoa huo kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na unyanyasaji vinavyotokea katika jamii zao ili serikali iweze kuchukua hatua sitahiki.
Mkuu wa mkoa aliongeza kuwa,jumla ya shilingi milioni 588,252.2 zimetolewa kwa vikundi 93 kutoka mapatao ya ndani ya Halmashauri za mkoa wa Ruvuma ambazo zimewezesha wananchi waliomo kwenye makundi maalum ya vijana,wanawake na wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.
Awali katika risala yao iliyosomwa na Amina Tindwa,wanawake wa mkoa huo wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutambua mchango wa wanawake na kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi ambazo zimewezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuondokana katika umaskini.
Wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuwawezesha wanawake kuonekana kwenye maeneo mbalimbali ya kisiasa,kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
Hata hivyo alisema,bado kuna kundi kubwa la wanawake limeachwa nyuma kutokana na rasilimali chache zinazopatikana ikilinganishwa na idadi ya wanawake waliopo.
Ameiomba serikali kulitupia macho kundi hilo na kushauri wanawake washirikishwe katika nafasi za maamuzi na kutatua changamoto zao kwenye maeneo na kutolea mfano utambuzi wa haki zao za msingi katika maeneo wanayoishi.
Tindwa ametolea mfano wanawake wa mkoa wa Ruvuma kuwa ndiyo wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula na biashara,lakini mara nyingi hawashirikishwi katika kupanga matumizi ya kile kinachozalishwa.
Alisema,jambo hilo limepunguza ari ya kufanya kazi kwa bidii hasa ya uzalishaji mali na hatimaye kusababisha uchumi wa kaya husika kudorora, tofauti na kaya ambazo wanashirikiana katika kupanga mipango bora ya maendeleo.
Ameishauri serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma,kutilia mkazo mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na Halmashauri za wilaya kwa makundi maalum ya wanawake,vijana na walemavu itolewe kwa wakati ili iweze kusaidia katika kukuza mitaji na kuongeza kipato cha familia.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo alisema,baadhi ya wanawake wanakosa huduma muhimu kutoka kwa waume zao kwa sababu ya wanaume kutumia muda wao mwingi wakiwa katika starehe.
Alisema,tabia hiyo imeleta maumivu makubwa kwa wanawake wengi na wengine wamekata tamaa na hata kujilaumu kwa kukubali kuingia kwenye ndoa ambazo zimepelekea kupata maumivu makubwa na kukosa furaha ,amani na utulivu katika maisha yao.
Mangosongo,amewataka wanaume kubadili na kusaidiana na wanawake kulea familia zao ili kujenga familia bora na kuwa na kizazi chenye furaha na utulivu wakati wote.