KAIMU Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya nafasi za kujiunga na Jeshi hilo leo Machi 9,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeatangaza nafasi za kujiunga na Jeshi kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya kuanzia Kidato cha Nne hadi Shahada ya Uzamili ambao wamemaliza Mkataba wa Mafunzo ya Kujitolea JKT na kurudishwa majumbani .
Hayo yamesemwa leo Machi 9,2023 jijini Dodoma Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda,wakati akitoa taarifa ya nafasi za kujiunga na Jeshi hilo kwa waandishi wa habari .
Luteni Kanali Ilonda ,amesema nafasi hizo zinawahusu vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha 4 na cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.
”Mwombaji anatakiwa awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa mwenye Kitambulisho cha Taifa, awe na umri wa miaka 18 hadi 26 kwa wenye elimu ya kidato cha nne hadi kidato cha sita na umri usiozidi miaka 27 kwa wenye elimu ya juu.”amesema Luteni Kanali Ilonda
Aidha amesema kuwa Mwombaji anatakiwa awe na afya nzuri na akili timamu, Mtanzania mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai Mahakamani na kufungwa pia asiwe ameoa au kuolewa.
Amesema anatakiwa awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na vyeti vya Taaluma, awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo pia awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa kujitolea miaka miwill (2) na kutunukiwa cheti.
Hata hivyo ameeleza kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia tarehe ya tangazo hili hadi tarehe 20 Machi, 2023 yakiwa na viambatisho ikiwemo nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA.
”Viambatisho vingine ni nakala ya cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shule na chuo, nakala ya cheti cha JKT pamoja na namba ya simu ya mkononi ya mwombaji.”amesema
Aidha ametoa onyo kwa wale wote watakaojihusisha na utapeli wowote kuelekea zoezi hili huku akisisitiza kuwa maombi yote yatumwe kupitia anuani ya;Mkuu wa Utumishi, Makao Makuu ya Jeshi,
Sanduku la Posta 194, DODOMA, Tanzania au katika barua pepe ya [email protected]
”Baada ya tangazo hili kuna mwanya wa matapeli utaibuka na watapenda kutumia fursa hii, nawaomba Watanzania kukataa kurubuniwa kwani hakuna njia ya mkato katika kupata nafasi hizi.”amesisitiza Luteni Kanali Ilonda