Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MKOA wa Pwani, kupitia madawati ya ustawi wa Jamii na maeneo ya utoaji huduma za kijinsia katika Halmashauri yamepokea migogoro ya ndoa 689 ,matunzo 908 na migogoro inayohusu watoto wa nje ya ndoa 973 katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2022 .
Kufuatia migogoro na mashauri hayo, ndani ya jamii, Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Halima Okash, akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake kimkoa yaliyofanyika Bagamoyo,alitoa rai kwa wanawake kupigania haki zao ,na kusisitiza Serikali ipo nyuma yao kuchukua hatua kwa wale ambao wanajaribu kuchezea haki za mwanamke na mtoto.
Aidha, aliiasa Jamii Mkoani humo kuendelea kulinda amani ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Okash alieleza,wanawake wamekuwa injini ya mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na wamekuwa mchango mkubwa katika kulea na kuelekeza maadili mema ya kitanzania kwa maana hiyo umoja na uzalendo uwe nguzo kimkoa na Taifa kijumla.
“Mkoa una Jumla ya kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zipatazo 546, jumla ya mashauri 2,570 yamepokelewa na kusikilizwa katika madawati ya ustawi wa jamii na maeneo mengine ya utoaji wa huduma katika Halmashauri kwa kipindi hicho, kati ya hayo migogoro ya ndoa 689,matunzo 908, watoto nje ya ndoa 973,yaliyopelekwa mahakamani 162 na yaliyohukumiwa 49″alifafanua Okash.
Kuhusu kumwezesha mwanamke,Okash alieleza, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 mkoa ulitenga kiasi cha sh Bilioni 3.6 hadi Januari 2023 ambapo Jumla ya Bilioni 1.5 zilichangiwa na kupelekwa kwenye akaunti ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, katika fedha hizo million 750,554,502 zilitolewa kwenye vikundi hivyo.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake Mkoani Pwani Zainabu Vullu aliyataka madawati ya kijinsia kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa jamii ili kudhibiti vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Aliwataka wanawake, wawa wabunifu na kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwani ni chachu katika kuleta usawa wa kijinsia pamoja na kutumia teknolojia vizuri ili kupata elimu ya kuandaa bidhaa Bora na kupata masoko.
Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake Mkoani Pwani, Mariam Ulega alieleza, wameanzisha Kampuni ya Gomama ili kumwezesha kiuchumi mwanamke na amewaomba wajiunge kununua hisa .
Mariam,aliwasisitiza wanawake hao kuendelea kujiinua kimaisha na kiuchumi ili kujiongezea kipato.
Mjasiriamali Rosemary Kwilasa aliishukuru Serikali kwa kutoa mikopo ya asilimia 10 katika mapato ya halmashauri ambapo kikundi Chao kilichopo Ukuni, Bagamoyo kimenufaika kwa kupatiwa milioni 8.