Kikundi cha wanawake wanaofanya kazi kwenye mgodi wa STAMIGOLD (UWASTAMI) uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera wameadhimisha sherehe za siku ya mwanamke duniani kwa kutoa vifaa muhimu katika maeneo ya kutolea huduma za afya kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Katika kuadhimisha sherehe hizo, wanawake hao wametembelea zahanati zilizopo kwenye vijiji viwili vya Mavota na Mkunkwa vilivyopo kata ya Kaniha na kubaini changamoto zinazowakabili mama na mtoto kwenye zahanati hizo na kuamua kusaidia baadhi ya vifaa.
Vifaa vilivyotolewa na wanawake hao ni vitanda 8 vya kujifungilia, magodoro 8, matenki ya maji 4, vifaa vya usafi, battery ya solar kwa ajili ya kutoa mwanga wakati wa usiku kutokana na vijiji hivyo kutokuwa na nishati ya umeme.
Vifaa vingine walivyovitoa wanawake hao katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani zilizofanyika viwanja Nyakahura Mzani ni tauro za kike kwa wanafunzi 250 wa shule za sekondari za Nyakahura na Mzani ambapo vifaa vyote hivyo vinagharama ya Zaidi ya shilingi milioni 7.7.
Hata hivyo wanawake hao wamewasihi wanawake wengine kutokuwa tegemezi na badala yake wajishughulishe sambamba na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotangazwa huku wakimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini wanake katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.