KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis akizungumza na waandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Chama na Serikali kes ujumla.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, kimevitaka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini kuacha tabia ya kuwapotosha wananchi juu ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya nane ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Kamis Mbeto Khamis, wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
Alisema kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wameanza kutumia vibaya fursa ya mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa kubeza na kutoa matamshi yasiyofaa juu ya masuala mbali mbali ya serikali.
Alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya nane imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuona maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati bila ya kuangalia, chama, dini rangi wala kabila la mtu.
Alisema, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Trilioni Moja katika kutekeleza Miradi mikubwa ya Maendeleo katika nyanja tofauti tofauti.
Alifahamisha kuwa,Chama cha ACT-wazalendo wamekuwa wakihubiri chuki,malumbano na sio kubishana kwa hoja jambo ambalo limekuwa likileta taswira mbaya na kuona lengo la kufunguliwa mikutao rasmi ya hadhara kutofikiwa.
Mbeto, alisema, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa dhamira yake kuu ni kuona vyama vinapiga kampeni zao kistarabu na kuwahamasiha wanachama wake kuona vyama vyao vinaendelea kupata wanachama na sio kukosoa uongozi uliokuwepo kama walivyofanya viongozi wa chama cha ACT Wazalendo.
Alisema, mategemeo ya CCM kuona wapinzani wa Tanzania wanaendelea kuikosoa serikali inayoongizwa na Chama cha CCM kwa hoja na kwa utaratibu kwa lengo la kuona hayo maendeleo yanafikiwa na sio kwa vurugu kama walivyolianzisha chama hicho.
Hivyo, aliwataka wanasiasa kufuata misingi na dhamira iliyowekwa na Rais Dk. Samia ya kuendelea kuhumiri amani na endapo wanapotaka kukosoa serikali kufanya kwa njia ya kistarabu na sio kuwatukana viongozi wa nchi jambo ambalo linapeleka kuingia katika matatizo.
“Mwenyekiti wetu Dk. Samia kwa muda mrefu alipokea maoni, ushauri wa kuruhusu harakati za siasa ziendelee nchini, na kama tunavyohamu muda ulizuiliwa kwa lengo la Chama kilichoshinda kuweza kufanya shughuli zake za amendeleo na kwa hekima alikutana na wadau akatafakari na kuona ni vyema kufanya shughuli zao za kisiasa” alisema
“Hatukatai kukosewa sisi kwani sio wakamilifu lakini wanapotukosoa wawe na hoja za kutosha na sio kurusha maneno yasiyoeleweka” alisema.
Mbali na hayo, Mbeto, alisema CCM imepiga hatua kwa kuwapelekea wannachi maendeleo kwa asilimia kubwa katika miaka miwili kwani maendeleo yamekuwa yakioneakana kwa vitendo bila ya kificho.
Alisema, katika utawala wa Dk. Mwinyi, Hospitali kubwa za wilaya zimejengwa katika mkoa yote ya Unguja na Pemba na maendeleo mbalimbali ikiwemo barabara, skuli na huduma za maji safi na salama katika mikoa mbaimbali.
“Dk. Mwinyi dhamira yake kuu ni kuona maendeleo yanafikiwa kwa wananchi wote hivyo CCM hatuna budi kumpongeza kwani pia ameonesha ukomavu wa kisiasa kwani hasikilizi maneno anafanya kwa vitendo” alisema.
Aidha Mbeto aliwataka Wanasiasa kuacha kupotosha na kufanya siasa za kistaarabu kwa mustakabali wa Taifa.