Mhandisi Dastan Sinkonda wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji akitoa maelezo kwa waandishi wa habari waliotembelea Mradi wa Bwawa la Maji Masaka mkoani Ringa
Mhandisi Dastan Sinkonda wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji akitoa maelezo kwa waandishi wa habari waliotembelea Mradi wa Bwawa la Maji Masaka lilopo wilayani Iringa
Muonekano wa Bwawa la Maji Masaka ulivyo kwa sasa baada ya ujenzi wake kukamilika Novemba 20222
************************
Na Selemani Msuya, Iringa
BODI ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB), imetumia Shilingi bilioni 1.7 kujenga Bwawa la Maji kata ya Masaka mkoani Iringa, hali ambayo inaenda kuondoa kero ya maji na kuchochea utunzaji wa mazingira.
Hayo yamesemwa na Dastan Sinkonda, Mhandisi Rasilimali za Maji RBWB, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Maji kata ya Masaka wilayani Iringa.
Sinkonda amesema bodi imejenga bwawa hilo baada ya kufanya utafiti na kubaini uwepo wa uhaba wa maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mifugo, uvuvi na kilimo katika kata hiyo ya Masaka.
Amesema bwawa hilo lilogharimu Sh. bilioni 1.7, litanufaisha wananchi zaidi ya 12,000 wa vijiji vya Sadani, Makota na Kaning’ombe na kuwataka wananchi kulitunza ili liwe endelevu.
“Ujenzi wa bwawa hili la Masaka ulianza Mei 2022 na kukamilika Novemba 2022, umegharimu Sh.bilioni 1.7 na matarajio ni eneo hili kujaa ndani ya miaka miwili iwapo mvua zitanyesha vizuri,” amesema.
Mhandisi huyo amesema ukubwa wa bwawa hilo ni mita za ujazo 439,000, urefu wa mita 260 na kimo cha mita 14, hivyo ni imani yao kuwa bonde litakuwa limetatu changamoto katika sekta ya jamii, kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa upande wake Diwani wa kaya ya Masaka Methew Nganyangwa amesema uamuzi wa Serikali kupitia Bonde la Rufiji kujenga bwawa hilo unaenda kutafsiri Tanzania ya viwanda kivitendo.
Amesema kitendo cha Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Sh.bilioni 1.7 za ujenzi wa bwawa hilo la kisasa unaenda kuchochea shughuli za kiuchumi katika kata hiyo kukuwa kwa kasi.
“Mradi huu wa Bwawa la Masaka unaenda kuondoa uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira ambao umekuwa ukifanywa na wananchi ambao walikuwa wanafanya shughuli za kilimo na nyingine kujipatia kipato.
Ni wazi kuwa maji kutoka katika vijito vya asili yatatiririka muda wote, hali ambayo itachangia uzalishaji wa umeme kwa asilimia 100 kwenye vyanzo vyetu vya Mtera, Kihansi, Kidatu na Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP),” amesema.
Nganyangwa ameitaka Serikali kuendelea kuwekeza katika miradi kama hiyo, ili dhamira ya kubadilisha maisha ya wananchi iweze kutimia kwa haraka.
“Hiki kinachofanywa na RBWB ni tafsiri sahihi ya uchumi wa viwanda ambao umekuwa ukipiganiwa na kila kiongozi ambaye amepata nafasi ya kuongoza nchi,” amesema.
Naye Betina Chang’a, Mkazi wa kijiji cha Makota kata ya Masaka amesema mradi huo utakuwa na manufaa zaidi kwa kina mama ambao wanajihusisha na shughuli za nyumbani na kilimo.
Amesema bwawa hilo litawaongezea kasi ya uzalishaji, hivyo uchumi wao utakuwa kwani kuna soko la uhakika la mazao mchanganyiko katika mkoa huo.
Chang’a amesema upatikanaji wa maji ya uhakika utachangia wao kufuga mifugo kama mbuzi ambao watawezesha kuuza na kujipatia kipato.
“Mwanamke akiwa imara kiuchumi, jamii nayo inakuwa imara, kata yetu ya Masaka ipo kilomita 30 kutoka Iringa mjini, tunaamini tutauza mazao yetu kwa uhakika, hivyo nitumie nafasi hii kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwapatia fedha, kwa ajili ya mradi huu,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji Bonde la Mto Lukalama, Onesmo Nzulumi amesema mradi huo unaenda kuweka usalama vyanzo vya maji katika kata hiyo ambayo vilikuwa vinaharibiwa kila siku.
“Eneo letu ambalo lina vijiji zaidi ya vitatu linaenda kuwa salama katika mazingira, hivyo maji yatatiririka kwa mwaka mzima na kwamba wamejipanga kuvilinda vyanzo vya maji kwa nguvu zote,”amesema.