Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Bw.Kaimu Mkeyenge, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 7,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TASAC, pamoja na kuelezea Mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
MKURUNGEZI Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Zamaradi Kawawa,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Bw.Kaimu Mkeyenge, kuwasilisha utekelezaji i wa majukumu ya TASAC, pamoja na kuelezea Mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Machi 7,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),limefanikiwa Kuboresha ufanisi wa bandari kwa kupunguza uwezo wa shehena inayoruhusiwa kukaa bandarini kwa wakati mmoja (yard density) kutoka asilimia 65 hadi asilimia 50 kwa kuweka Amri ya Tozo ya Bandari Kavu.
Hayo yameelezwa leo Machi 7,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw.Kaimu Mkeyenge wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TASAC, pamoja na kubainisha Mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bw.Mkeyenge amesema kuwa wamefungua ofisi 11 za Shirika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma karibu na wananchi Shirika lina ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Rukwa, Ukerewe pamoja na Geita.
Mkeyenge ametaja mafanikio mengine kuwa ni Kuwashirikisha wadau katika maamuzi ya kiudhibiti na masuala mengine yanayowahusu ili kuimarisha mahusiano.
Mafanikio mengine ni kuwezesha ongezeko la idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na TASAC ambapo idadi ya leseni na vyeti vya usajili ilifikia 1,195 kwa mwaka wa fedha 2021/22 ikilinganishwa na leseni na vyeti vya usajili 941 katika mwaka wa fedha 2018/19 sawa na ongezeko la asilimia 79.
“TASAC imewezesha ongezeko la idadi ya vyeti vya mabaharia waliokidhi masharti kutoka 6,068 katika mwaka 2018/19 hadi kufikia 19,575 katika mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 31,”amesema Mkeyenge.
Aidha Mkeyenge amesema TASAC imeweza kuimarisha usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira dhidi ya shughuli za meli ili kupunguza matukio ya ajali za vyombo vya majini ambapo kaguzi za vyombo vya usafiri majini zilifanyika 6,208 katika mwaka wa fedha 2021/22 na kaguzi 4,490 katika kipindi cha Julai 2022 mpaka Januari 2023 inayotarajiwa kufikia vyombo takriban 8,000 ifikapo mwezi Juni 2023.
Mkeyenge ametaja fursa zinazopatikana katika sekta ya usafiri majini ambazo zinaweza kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kusajili meli kwa masharti nafuu (open registry).
Ametaja fursa nyingine kuwa ni kuanzisha maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ukanda wa pwani, kuanzisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa pwani, kuanzisha viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki na kujenga bandari rasmi za uvuvi.
TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018. Kuundwa kwa TASAC ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususan kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji. Hii ni kwa sababu Tanzania ina ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi wenye urefu takriban Kilomita 1,424, Maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa