**************************
Kassim Nyaki na Samwel Nsyuka, Berlin.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi zinazoshiriki katika maonesho makubwa ya Utalii Duniani (International Tourism – Börse Berlin) yanayofanyika katika jiji la Berlin Nchini Ujerumani kuanzia tarehe 7-9 Machi, 2023 ambapo mataifa 180 yanashiriki maonesho hayo.
Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki maonesho hayo unaongozwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Shirika la ndege Tanzania (ATC) pamoja na kampuni 58 kutoka Sekta binafsi nchini Tanzania zinashiriki maonesho hayo.
Balozi wa Tanzania Nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameeleza kuwa maonesho ya ITB Berlin ni maonesho makubwa na muhimu kwa wadau wa sekta ya Utalii duniani kukutana na kuuza bidhaa za utalii ambapo nchi ya Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yenye wageni wengi wanaoitembelea Tanzania.
“Ushiriki wa Tanzania katika maonesho haya ni muhimu sana katika kuendelea kutangaza vivutio vya Utalii pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania, Taasisi za Serikali na makampuni ya sekta binafsi takribani 58 yaliyopo katika maonesho haya yamepata nafasi ya kutangaza bidhaa zetu na kuongea wadau wa utalii katika nchi za ulaya kuhusu huduma tunazotoa na kupata na maoni na mahitaji yao ili kuboresha huduma tunazotoa kwao” ameongeza Dkt. Possi.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Ubalozi wa Tanzania Nchini Ujerumani inaendelea na jitihada za kuitangaza Tanzania katika taifa la Ujerumani na nchi jirani ikiwemo Poland, Austria na Jamhuri ya Czech ili kuongeza mara dufu idadi ya watalii kwa kuwa Nchi ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira wezeshi hasa kuboresha miundombinu ya Utalii katika maeneo mbalimbali ya Hifadhi zetu baada ya uzinduzi wa filamu ya Tanzania the Royal tour.
Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo kale Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said amewapongeza Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kwa kutoa hamasa kwa Makampuni ya Utalii kutoka Tanzania kushiriki maonesho hayo.
“Hamasa hii imesaidia kupanua wigo wa kupata masoko mapya ya ukada huu wa nchi za Ulaya mashariki , lakini pia nchi za Nordic hasa Sweden, Finland, Norway ambazo watu wao tuko nao katika maonesho haya na inasaidia kuuza bidhaa za Tanzania kwao kupitia majukaa mbalimbali tunayofanya katika maonesho haya”
Mhe. Simai amebainisha kuwa hamasa ya ushiriki ya makampuni ya sekta binafsi kutoka Tanzania katika maonesho hayo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt Hussen Mwinyi kupitia filamu ya Tanzania the Royal Tour kuwa mabalozi wa nchi na vivutio vyetu
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania Bw. Damas Mfugale ameeleza kuwa mbali na na Taasisi za Serikali zinazoshiriki maonesho hayo idadi ya kampuni kutoka sekta binafsi ikatika sekta za bodi za watalii, hoteli waendeshaji wa utalii, watoa huduma ya utalii, mashirika ya ndege na kampuni za kukodisha gari wanashiriki maonesho hayo.
Mfugale ameeleza kuwa Tanzania kushiriki maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa Nchi kujitangaza kwenye masoko ya kimkakati ambapo Tanzania bara na Zanzibar wanaandaa mkakati wa pamoja kuitangaza Tanzania kupitia bidhaa zake za vivutio mbalimbali vya utahii katika hifadhi zetu na utalii wa fukwe kwa upande wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa jarida la takwimu za Utalii la mwaka 2021 zaidi ya wageni 67,284 kutoka nchi ya Ujerumani wanatembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania.