Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo, Balozi Dk. Pindi Hazara Chana wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 7,2023 jijini Dodoma kuhusu Serikali kuridhia kumlipa Mshahara Kocha Mkuu wa Taifa Stairs
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) Adel Amrouche,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 7,2023 jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Wizara Utamaduni, Sanaa na Michezo ,Saidi Yakubu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 7,2023 jijini Dodoma kuhusu Serikali kuridhia kumlipa Mshahara Kocha Mkuu wa Taifa Stairs
Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wilfred Kidao ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 7,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kuendeleza Mchezo wa Soka nchini Serikali imeridhia kumlipa mshahara wa kocha wa Timu ya Taifa Stars,Adel Amrouche ambae ataongoza kikosi hicho katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Hayo yamesemwa leo Machi 7,2023 jijini Dodomana na Waziri wa Utamaduni,Sanaa na michezo, Balozi Dk. Pindi Hazara Chana wakati akizungumza na waandishi wa habari
Dk.Chana amesema kuwa Serikali inaamini Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limejiridhisha na ubora wa kocha huyo ambaye ataweza kukuza Soka la Tanzania hivyo bajeti yake itazingatiwa na Serikali
”Ukitazama wasifu wa Kocha Adel utabaini uzoefu mkubwa alionao katika bara la Afrika na pia kuandaa wataalamu wengine hivyo tumtumie vizuri na tumpe ushirikiano ili aweze kuisaidia timu yetu kufanya vizuri ndani na nje ya nchi”amesema Dk.Chana
Aidha amesema kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kupata wataalamu wengine katika michezo mingine pamoja na kuimarisha wanamichezo kupitia kituo cha maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Kwimba Mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wilfred Kidao amesema kuwa wametumia kigezo cha uzoefu katika bara la Afrika katika kufundisha mpira wa Miguu hivyo ataweza kuleta mabadiliko makubwa katika soka nchini.
Kidao amesema kuwa Amrouche raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika baada ya kufundisha klabu na timu za taifa katika ukanda Kusini, Mashariki, Kati na Kaskazini.
”Amewahi kuwa Kocha Bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013 wakati akiinoa na kuipa Kenya, Harambee Stars Ubingwa wa Cecafa Challenge pamoja na kuweka rekodi ya Harambee Stars kucheza mechi 20 bila kupoteza na kuifikisha nusu fainali mara mbili akiwa na Burundi.”amesema Kidao
Kocha Amrouche amewahi pia kuzinoa timu za taifa za Equatorial Guinea, Botswana, Libya na Yemen kwa nyakati tofauti.
Aidha amefundisha timu mbalimbali kama DC Motema Pembe,RC Kouba, USM Alger, alizowahi kuzichezea na MC Algiers, zote za Algeria.
Aidha, Kocha Adel ni mkufunzi wa walimu wa Pro Licence wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) akizalisha makocha wengi bora barani Afrika na ana uzoefu mkubwa katika soka la vijana, kazi aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 10 nchini Algeria na Ubelgiji.
Naye Kocha Adel Amrouche amewataka wachezaji wa Tanzania kuona thamani ya kuichezea timu ya taifa ili waweze kuipatia heshima nchi hivyo anaomba ushirikiano kutoka kwa wadau katika kufanikisha kazi yake.