Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Watendaji (hawapo pichani) kuhusu kuboresha utendaji kazi katika kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Watendaji kuhusu kuboresha utendaji kazi katika kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.
**************************
Na Happiness Shayo
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameongoza kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na hatimaye kukuza utalii na kuimarisha usimamizi wa Uhifadhi wa Maliasili nchini.
Kikao hicho kimefanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.
Mhe.Masanja ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Taasisi kuwa wabunifu kwa kutumia historia ya taifa na elimu ya viumbe hai kuwa fursa ya kujifunza na kuiongezea Serikali Mapato na kuongeza ajira na kipato kwa Mwananchi mmoja mmoja.
Aidha, kikao hicho kilijadili namna ya kutumia Makumbusho za Taifa kama eneo mojawapo la kuiongezea Serikali mapato kwa kuwa wana wigo mpana zaidi kuliko Taasisi nyingine katika kuibua fursa zilizopo nchini.
Katika hatua nyingine, Mhe.Masanja amekielekeza Chuo cha FITI kuandaa mpango utakaokiwezesha Chuo hicho kuwepo na miradi mbalimbali itakayokiwezesha kuongeza mapato kwa njia ya Mafunzo.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Makumbusho ya Taifa ( NMT) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.