Dar es Salaam- 06 Machi, 2023
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza akimwakilisha Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, leo tarehe 6 Machi, 2023 ameungana na Waombolezaji katika Misa ya Kuuaga Kijeshi Mwili wa aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (1995-1996) Martine K. Mbago nyumbani kwa marehemu Chanika Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi, Kamishna Semwanza alisema Marehemu Kamishna Mstaafu Mbago, alitumikia vyema na ni miongoni wa Waanzilishi ambao wamelitengeneza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa na mwonekano huu tunaouona hii leo, na kuongeza kuwa Marehemu alifanya kazi kwa Uaminifu na kwa Weledi na kuwatengeneza Maafisa na Askari ili kuja kulitumikia Jeshi katika Huduma za Kuzima Moto na Uokoaji.
“…Kwa Ujumla, Marehemu alifanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, amewatengeneza Askari na Maafisa ili kuja kulitumikia Jeshi na Taifa kwa ujumla katika huduma za Kuzima Moto na Uokoaji katika dharura mabalimbali…” alisema Kamishna Semwanza.
Katika Misa hiyo ya Kuuaga mwili wa Kamishna Mbago, Viongozi mbalimbali walihudhuria ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Benard Mchomvu, Makamishna Wastaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania bara na Kamishna Mstaafu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Ali Malimusy.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa shukurani za dhati kwa wote waliohusika katika kufanikisha zoezi la mazishi ya Mwili wa Marehemu.
(Picha zote na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)