*********************
? AONGOZA VIKAO VYA MABORESHO NA TAASISI ZAKE KWA ZAIDI YA MASAA 10
Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Machi 5, 2023 ameongoza vikao vya maboresho na Watendaji na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa zaidi ya masaa kumi kujadili na kufanya mapitio mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa raslimali kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Katika vikao hivyo vilivyofanyika jijini Arusha, Mhe. Mchengerwa ameambatana na Naibu wake Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, na Naibu Katibu Mkuu, Anderson Mutatembwa ambao pia wamepata fursa ya kushiriki kikamilifu katika kupitishwa kwenye sheria, kanuni na masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi na usimamizi wa rasilimali kwenye taasisi hizo.
“ Tumefanya mapitio na Watendaji wa wizara hii hasa Wakuu wa Taasisi ambazo zipo chini ya wizara hii na kufanya mapitio ya kina kabisa kwa siku nzima ya leo ambapo tumeona namna taasisi hizo zilivyoanzishwa na mwelekeo wa wizara na tunakotaka kuelekea na misingi ya utekelezaji wa maelekezo ya viongozi lengo likiwa pia kujenga matumaini kwa wananchi wetu” amefafanua Mhe. Mchengerwa mara baada ya kumaliza vikao hivyo.
Aidha, amesema katika vikao hivyo pia wameweza kujadili kwa kina sheria, kanuni na utekelezaji wa kazi za kila siku kwa kuzingatia kuwa kumekuwa na mabadiliko kwenye taasisi nyingi hususani baada ya kubadili mifumo ya kiraia na kufuata ile ya kijeshi katika usimamizi wa raslimali ambapo amesisitiza kuwa kumekuwa na mapungufu kadhaa ya kufanyiwa kazi na ameshaagiza kufanyiwa kazi mara moja.
“Kumekuwa na mapungufu makubwa sana ya kisheria , lakini pia kumekuwa na mapungufu mengi kwenye kanuni ambayo yanahitaji maboresho makubwa, kwa hiyo tunapaswa kufanya marekebisho ya haraka ili tuweze kufanya kazi ya uhifadhi wa raslimali kwa ufanisi zaidi, tayari tumeshapeana muda wa kufanya marekebisho haya mara moja, yale yanayonihusu mimi moja kwa moja nitayakamilisha haraka kwa wakati” ameongeza Mhe. Mchengerwa
Aidha, amesema katika vikao hivyo wameweza kukumbushana maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na viongozi wa taasisi kuhakikisha kuwa wanatoka na kwenda kufanya vikao mbalimbali na wananchi wanaozunguka maeneo husika ili kutoa uelewa wa kuhifadhi raslimali.
Amewataka kuwa karibu na jamii na kujenga umoja na mshikamano na kuwashirikisha wananchi katika mipango ya kulinda mifumo anuai ya ikolojia katika uhifadhi wa raslimali hali ambayo amesema kama itaboreshwa itasaidia sana kwa kuwa baadhi ya changamoto zinazojitokeza ni kwa sababu taasisi hazipo jirani na wananchi wanaowazunguka.