Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na Misako na Doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni Pamoja na kukamata watuhumiwa wa wizi, dawa za kulevya na biashara za magendo. Aidha Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kwa Amani na Utulivu.
WATATU WANASHIKILIWA KWA KUINGIZA NCHINI VIPODOZI VYENYE VIAMBATA SUMU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu [majina yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi] wakazi wa Tunduma kwa tuhuma za kuingiza nchini vipodozi vya aina mbalimbali vilivyopigwa marufuku vyenye viambata sumu pamoja na bidhaa za magendo kupitia njia za panya.
Watuhumiwa wamekamatwa Machi 03, 2023 majira ya saa 12:30 asubuhi katika misako iliyofanyika huko maeneo ya Izumbwe, Wilaya ya Mbeya vijijini na kufanikiwa kuwakuta wakiwa na vipodozi vya aina mbalimbali vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini ambavyo ni:-
- CARORITE BOX 20
- CREAM AINA YA NAOMI CATON 10
- NEPROSONE GEL BOX 45
- CREAM PEAU CREIRE CATON 8.
- DIANA CATON LOTION 8,
- CREIRE FOR MEN CATON 12.
- DERMO GEL DAZAN 26,
- COCOPUP BOX 26
- MAFUTA AINA COCOPAP BOX 04.
- EPIDERM ZIPO CATON 9.
- VAROLIGHT BOX 2.
- BETASOL BOX 2.
- DERMO GEL 26
Aidha katika upekuzi, watuhumiwa walikutwa na mali Vitenge jola 26 vilivyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru wa forodha kupitia njia zisizo rasmi vikiwa ndani ya Gari namba T.165 BQT aina ya Cresta GX 100. Watuhumiwa walikuwa wakisafirisha vipodozi hivyo vyenye viambata sumu na Vitenge hivyo kwa kutumia gari yenye namba za usajili T.165 BQT CRESTA GX 100 kutoka nchini Zambia kupitia njia isiyo rasmi ya Ilembo Umalila. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
ATIWA MBARONI KWA KUKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshjikilia FILIMONI LAMBASIKA [38] Mkazi wa Sambilimwaya Wilayani Chunya kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi kiasi cha debe nne yenye uzito wa kilogramu 15.
Mtuhumiwa alikamatwa Machi 02, 2023 majira ya saa 07:30 mchana katika msako uliofanyika huko Kitongoji cha Sambilimwaya, Kijiji cha Chokaa, Wilaya ya Chunya. Mtuhumiwa alikamatwa akiwa anafanya biashara ya kuuza dawa hizo za kulevya akiwa ameifunga kwenye mifuko ya nailoni alimaarufu rambo na mfuko wa sandarusi.
AKAMATWA AKIWA NA MIFUGO YA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika muendelezo wa misako inayofanyika katika maeneo ya Mkoa wa Mbeya, linamshikilia HEWAD JACKSON [33] Mkazi wa Kijiji cha Ilembo Mbeya Vijijini kwa tuhuma za kupatikana na ng’ombe 10 wa wizi wenye thamani ya shilingi milioni kumi na tano [15,000,000/=].
Awali mnamo 02.03.2023 huko kijiji cha Ntokela kilichopo Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilimtilia mashaka mtuhumiwa baada ya kumuona akiwaswaga ng’ombe 10 na ndipo kumkamata na wakati akiendelea kuhojiwa katika ofisi ya Kijiji cha Ntokela alijitokeza mhanga aliyeibiwa ng’ombe zake aitwaye THADEO WILLIAM [50] Mkazi wa Kijiji cha Shango ambaye alizitambua ng’ombe hizo kuwa zimeibiwa huko kijiji cha Kikondo kilichopo Kata ya Ilungu Mbeya vijijini. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kujua watu anaoshilikiana nao katika matukio ya wizi wa mifugo Pamoja na kujua maeneo anayouza ng’ombe hao.
WITO:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wafanyabiashara kuachana na biashara za magendo na zile za bidhaa zilizopigwa marufuku nchini kwani watapata hasara, ni vyema kufanya biashara halali kwa ustawi wao na nchi kwa ujumla. Aidha tunatoa wito kwa wananchi kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini vyenye viambata sumu kwani ni hatari kwa afya zao. Pia tunatoa wito kwa yeyote aliyeibiwa ng’ombe, kufika kituo cha Polisi Tukuyu Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya utambuzi wa mifugo yake.
Imetolewa na,
BENJAMIN E. KUZAGA – ACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.
“Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu…Msingi wa Mafanikio Yetu”